Makampuni ya Uturuki yatachimba mafuta na gesi katika visima vya Pakistan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alisema wakati wa ziara rasmi mjini Islamabad.
Akizunguma wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Pakistan na Waziri wa Mambo ya Nje Muhammad Ishaq Dar siku ya Jumatano, Fidan alisisitiza kuwa nia ya Uturuki ni kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nishati na Pakistan, hasa katika sekta za kimkakati.
"Uturuki na Pakistan wanafanya kazi pamoja kwa lengo la kuimarisha kiwango cha biashara hadi dola bilioni 5," Fidan alisema. "Pia tunatathmini ushirikiano katika maeneo muhimu ikiwemo madini, mafuta, gesi asilia, na vile vinavopatikana ardhini."
Fidan alieleza kuwa makubaliano ya nishati yaliyotiwa saini mwezi Aprili kati ya Shirika la Petroli la Uturuki (TPAO) na Kampuni ya kitaifa ya mafuta ya Pakistan kuwa “ni hatua muhimu ya maendeleo” kwa lengo la kuimarisha ushirikiano.
Kutokana na makubaliano haya, Makampuni ya Uturuki na Pakistan yatashirikiana katika uchimbaji wa mafuta na gesi katika maeneo ya Pakistan—jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya ushirikiano wa nishati kati ya Uturuki na Pakistan.
“Hii ni moja ya matokeo ya mtazamo huo wa kitaasisi ambao tunalenga kuanzisha,” aliongeza.
Kuimarisha ushirikiano
Ishaq Dar alisema Pakistan na Uturuki wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbali mbali, ikiwemo uchumi, sekta ya ulinzi, nishati, na miundombinu.
Akipongeza sekta ya ulinzi ya Uturuki, Dar alisema Pakistan inalenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na katika sekta ya ulinzi pamoja na kuendeleza amani na uthabiti katika kanda.
Pande zote hizo mbili "kwa dhati kabisa" zinashirikiana katika masuala mbali mbali, ikiweo kubadilishana mawazo ya kukabiliana na ugaidi, alisema Dar.
Makampuni ya Uturuki pia yatashiriki katika ubinafsishwaji wa sekta ya umeme, aliongeza.
Maeneo maalumu ya kiuchumi
Pande zote mbili, Dar alisema, zinafuatilia kuanzishwa kwa maeneo maalum ya kiuchumi kwa ajili ya wajasiriamali katika miji ya Karachi na Istanbul.
"Tunafuatilia kuhusu kufaidika kutoka kwa uzoefu wa Uturuki na utaalamu wao katika masuala ya biashara ya meli, na matumizi sahihi ya maji kwa ajili ya kilimo," Dar alisema.
Alisema Pakistan na Uturuki wamekubaliana kuhusu tume ya mawaziri ya pamoja baada ya miaka 11, ambayo itakuwa na wenyeviti wenza Waziri wa Biashara wa Pakistan Jam Kamal na Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Yasar Guler.
"Juhudi zote hizi zitaweka msingi wa kongamano la nane la Baraza la Ushirikiano wa Kimkakati," ambalo litafanyika mwaka ujao nchini Uturuki, aliongeza.