Sudan Kusini ilisema Jumanne kwamba wahamiaji wanane waliofukuzwa na kupelekwa katika taifa hilo la Kiafrika na utawala wa Trump kwa sasa wako chini ya uangalizi wa mamlaka huko Juba baada ya kushindwa katika juhudi za kisheria za kusitisha uhamisho wao katika nchi hiyo isiyo na utulivu wa kisiasa.
Wanaume hao, ambao walikuwa wamezuiliwa na Marekani kwa zaidi ya mwezi mmoja katika kambi ya kijeshi nchini Djibouti, walifukuzwa siku ya Ijumaa na kuwasili katika mji mkuu wa Sudan Kusini Jumamosi, serikali ya Marekani na maafisa wawili katika uwanja wa ndege wa Juba walisema.
Wanaume hao wanafanyiwa uchunguzi kwa mujibu wa sheria za Sudan Kusini na kanuni zinazotumika za kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje ilisema katika taarifa yake, na kuongeza kuwa serikali ya Juba imejibu ombi la Marekani la kuwachukua wahamiaji hao "kama ishara ya nia njema."
Hatima ya wahamiaji hao imekuwa kizungumkuti katika vita juu ya uhalali wa kampeni ya Rais Donald Trump ya kuzuia uhamiaji kupitia uhamisho wa hali ya juu hadi "nchi za tatu" ambapo wahamiaji wanasema wanakabiliwa na wasiwasi wa usalama.
Wanaume hao wanane, ambao, kwa mujibu wa mawakili wao, wanatoka Cuba, Laos, Mexico, Myanmar, Sudan na Vietnam, walikuwa na hoja kwamba kufukuzwa kwao Sudan Kusini kungekiuka Katiba ya Marekani, ambayo inakataza adhabu ya kikatili na isiyo ya kawaida.