Shirika la Habari la Marekani, Associated Press (AP), liliripoti Jumanne kwamba Israel inafanya mazungumzo na taifa la Sudan Kusini kuhusu uwezekano wa “kuwahamisha” Wapalestina wa Ukanda wa Gaza kwenda nchi hiyo ya Afrika Mashariki, kama sehemu ya mpango wa kuwafurusha kwa lazima unaoendeshwa na Tel Aviv kwa msaada wa Marekani.
Kwa mujibu wa AP, ikinukuu watu sita walio na ufahamu wa suala hilo lakini wasiotaka kutajwa majina, “Mazungumzo hayo tayari yamefanyika kati ya Israel na Sudan Kusini, taifa linalokabiliwa na mgogoro wa kifedha na ambalo limepitia vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi. Hata hivyo, haijulikani hatua imefikia wapi.”
Hadi sasa hakuna majibu kutoka kwa mamlaka za Sudan Kusini kuhusiana na taarifa hizo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ilikataa kutoa maoni, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Kusini hakujibu maswali kuhusu mazungumzo hayo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema Wizara hiyo haitoi maoni juu ya mazungumzo ya kidiplomasia ya faragha.
AP ilibainisha kwamba “mazungumzo haya yakigeuka kuwa makubaliano rasmi, yatasaidia Sudan Kusini kujenga uhusiano wa karibu zaidi na Israel.”
Wakati huo huo, gazeti la Kiebrania Yedioth Ahronoth liliripoti kuwa Israel inaendesha mazungumzo na nchi tano, ikiwemo Sudan Kusini, kuhusu kupokea wakimbizi wanaofurushwa kwa lazima kutoka Gaza.
AP iliongeza kuwa wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Kusini alitembelea Israel, ingawa haikutoa maelezo zaidi.