Kenya na Iran zimekubaliana kuunda kamati ya pamoja ambayo itafanya kazi ya kuondoa vikwazo vya kibiashara ndani ya siku 60, na hivyo kufungua njia ya kuondolewa kwa marufuku ya mauzo ya chai ya Kenya katika taifa hilo la Mashariki ya Kati.
Makubaliano hayo yalifikiwa wakati wa Kikao cha 7 cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Kenya na Iran (JCC) kilichofanyika Nairobi, kikiongozwa na Waziri Mkuu Musalia Mudavadi na Waziri wa Kilimo wa Iran, Dkt. Gholamreza Nouri Ghezalcheh.
Marufuku hiyo ilichochewa na madai ya biashara mbovu ya uhalifu iliyohusisha kampuni moja ya Kenya.
"Kabla ya matukio ya kusikitisha ambayo yalisababisha kusimamishwa kwa mauzo ya chai kwa Jamhuri ya Iran, nchi ilikuwa mojawapo ya waagizaji wakuu wa chai ya Kenya. Mauzo ya chai yaliongezeka kutoka tani 3.2 mwaka 2020 hadi rekodi ya juu ya tani 13 mwaka 2024, na thamani inayolingana ya dola milioni 5 mwaka 2030." alibainisha Waziri Mkuu wa Kenya Mudavadi.
"Ukuaji huu ulifikiwa licha ya bei kikomo ya dola 2 kwa kilo kwa chai ya Kenya ambayo ni ya daraja la juu ikilinganishwa na chai ya India na Sri Lanka iliyofikia dola 4.5 kwa kilo. Serikali ya Kenya inatazamia kuondolewa kwa marufuku hiyo ili uuzaji wa chai ya Kenya hadi Iran urejee," aliongeza Mudavadi.
Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe alisema serikali zote mbili zimeazimia kuanzisha kanuni kali ili kulinda uadilifu wa mauzo ya chai ya Kenya.
"Sekta ya chai ya Kenya ni mojawapo ya mapato yetu makubwa ya fedha za kigeni, na ni lazima tuilinde dhidi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wanaharibu sifa yetu," alisema.
Vikwazo hivyo vimesababisha madhara makubwa ya kiuchumi kwa wakulima na wauzaji bidhaa nje.
Kamati mpya ya pamoja iliyoundwa itaunda mfumo wa kurejesha imani, kutekeleza viwango vya ubora, na kurejesha mauzo ya nje kabla ya siku 60.
JCC ilitoa fursa kwa nchi hizo mbili kutathmini ushirikiano wa kina na kutengeneza njia mpya katika maeneo yanayoibukia kama vile kilimo kinachozingatia hali ya hewa, viwanda, usafiri na miundombinu, elimu na mafunzo, ushirikiano wa forodha hadi forodha na nishati mbadala miongoni mwa mengine mengi.