Shirika la Afya Duniani halichukulii tena mlipuko wa mpox barani Afrika kuwa dharura ya kiafya kimataifa, mkurugenzi wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa alisema siku ya Ijumaa.
Aina mpya ya mpox iliibuka mapema 2024 Congo na mataifa jirani ya barani Afrika, ikiambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine ikiwemo kujamiiana. WHO ilisema ilitangaza maambukizi hayo kuwa dharura ya kiafya duniani Agosti mwaka jana.
Mkurugenzi Mkuu Tedros Adhanom Ghebreyesus amewaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa kuwa kikosi kazi cha dharura kilichoundwa baada ya mlipuko kimeshauri kuwa hali hiyo siyo tena dharura kimataifa, na “Nimekubali ushauri wao.”
Tangazo la dharura ya kimataifa la WHO, idara ya juu zaidi ya kuonya kuhusu tishio la masuala ya afya, linaashiria kutolewa kwa raslimali na kuhamasisha umma miongoni mwa hatua nyingine.
‘Tishio bado lipo’
“Bila shaka, kuondolewa kwa tangazo la dharura haimanishi tishio limeondoka kabisa, na siyo eti tutaacha kuliangazia kabisa,” mkuu huyo wa WHO alisema.
Siku ya Alhamisi, Kituo cha Africa CDC kilisema Mpox bado ni sehemu ya afya ya dharura barani Afrika.
Katika taarifa, Africa CDC ilisema kundi la ushauri, ambalo linamshauri mkurugenzi mkuu wa Africa CDC kuhusu mpox, lilitoa wito kuwa Dharura ya Afya ya Umma itaendelea kuwepo kwa lengo la kuendeleza utashi wa siasa, na nchi kuendelea kuwa makini.
Ugonjwa tofauti
Mpox ni tofauti na inaambukizwa kwa virusi katika familia moja kama vile inavyoambukizwa ndui.
Imeenea katika baadhi ya maeneo barani Afrika, ambapo watu wanaambukizwa kupitia panya na wanyama wengine wadogo. Dalili za kawaida zinaweza kuwa homa, kutetemeka na maumivu ya mwili. Dalili mbaya zaidi, watu wanaweza kuwa na vipele usoni, mikononi, kifuani na sehemu za siri.