Salum Mwalimu kutoa ushindani kwa Samia?
Salum Mwalimu kutoa ushindani kwa Samia?
Katika kampeni zake, Salum Mwalim ameweka mkazo kwenye sekta ya kilimo, akiahidi kuiongezea nguvu kwa nia ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwezesha kuwa na uhakika wa chakula na mazao ya biashara.
tokea masaa 13

Miaka michache iliyopita, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kilikuwa na sura ya Mzee Hashim Spunda Rungwe na sera yake maarufu ya ‘ubwabwa kwa wote.’

Ilikuwa ni kawaida kumuona mzee huyo, ambaye ndie muasisi wa chama hicho akiwa amezungukwa na watu wachache kwenye kampeni zake na baadaye ‘kujichana’ wali, maharage na nyama baada ya mikutano ya kampeni.

Ila kwa sasa, mambo yamebadilika. Hasa baada ya kundi kubwa la waliokuwa wanachama na viongozi wa Chadema kuhamia Chaumma.

Hivi sasa Salum Mwalim ndiye sura halisi ya chama hicho kilichoanzishwa mwaka 2013.

Mwalim, ambaye ni mwandishi wa habari kitaluuma, ndie anayepeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi ya urais, kwa upande wa Tanzania Bara, huku akisindikizwa na Devotha Minja, ambaye pia ni mwanahabari, akiwa mgombea mwenza wake.

Itakumbukwa kuwa, Salum Mwalim alikuwa ni miongoni wa watu waliokihama chama cha CHADEMA, wakidai kutofurahishwa na mwenendo wa uongozi mpya wa chama chini ya Mwenyekiti wa wa sasa, Tundu Lissu, ambae anakabiliwa na kesi ya uhaini pamoja na makosa mengine.

Wengine waliokihama chama hicho ni pamoja na Benson Kigaila, John Mrema na Devotha Minja.

Ndani ya CHADEMA, Salum Mwalim alishika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ile ya unaibu katibu Mkuu kwa upande wa Zanzibar.

Aliwahi pia kufanya kazi katika kituo cha habari cha Chanel Ten.

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Mwalim, ambaye pia aliwahi kuwa meneja masoko wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, kuwania nafasi ya urais.

Mara ya kwanza ilikuwa ni wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, akiwa kama mgombea mwenza wa Tundu Lissu, kwa tiketi ya CHADEMA.

Katika kampeni zake, Salum Mwalim ameweka mkazo kwenye sekta ya kilimo, akiahidi kuiongezea nguvu kwa nia ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwezesha kuwa na uhakika wa chakula na mazao ya biashara.

Pia ameahidi kuwepo kwa nidhamu kwa kila mtumishi wa umma, na kuwaboreshea maslahi yao kwa kuanza na mshahara wa 800,000 kwa kima cha chini, ikiwa ni baada ya makato ya kodi.

Salum Mwalim amepigia chapuo sera ya habari ili vyombo vya habari vifanye kazi kwa weledi na kuifanya tasnia hiyo kuwa mhimili kamili kama ilivyo Mahakama, Serikali na Bunge.



CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us