AFRIKA
2 dk kusoma
Maulidi yaadhimishwa kwa sherehe kubwa Somalia
Somalia imetangaza siku ya Maulidi kuwa sikukuu ya kitaifa ili kuimarisha sherehe hizo, huku mikusanyiko ikiwa mikubwa zaidi kuliko miaka ya nyuma kutokana na hali bora ya usalama.
Maulidi yaadhimishwa kwa sherehe kubwa Somalia
Wasomali mjini Mogadishu wakisherehekea Maulid al-Nabi, siku ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad. / / Reuters
tokea masaa 18

Maelfu ya Wasomali wameandamana mitaani jijini Mogadishu kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad, ikiwa ni sikukuu iliyotangazwa rasmi na serikali.

Wizara ya Kazi na Masuala ya Kijamii ilitangaza siku hiyo kama mapumziko ya umma kwa wafanyakazi wa serikali na sekta binafsi kwa heshima ya tukio hilo.

Katika tarehe 12 ya Rabiul Awwal kwenye kalenda ya Kiislamu, Waislamu duniani kote hukusanyika kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad.

Kwa mwaka huu, siku ya Maulidi imeadhimishwa kote Somalia kwa kisomo cha Qur’an, kaswida za kidini, na zefe.

Sherehe kama hizo pia zimefanyika katika sehemu nyingine za ulimwengu wa Kiislamu.

Katika mji mkuu, Mogadishu, barabara zilifurika waumini, wengi wao wakiwa vijana waliovaa mavazi meupe na wakipeperusha bendera za kijani kibichi.

Makundi ya watu yalitoka misikitini na kujazana katika maeneo ya wazi wakitoa mashairi na kaswida za maadhimisho ya Mtume Muhammad, kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press.

Wanazuoni wa Kiislamu walikuwa wakisoma aya za Qur’ani kupitia vipaza sauti huku watu wakicheza kwa pamoja, wakipiga makofi na kushangilia kwa furaha.

Maulidi ina maana ya ndani kwa wengi

Baadhi ya vijana walirekodi mikusanyiko hiyo kwa simu zao na kupaza moja kwa moja kwa marafiki walioko nje ya nchi, huku wengine wakibeba mabango yenye maandiko ya sifa kwa Mtume.

Vikosi vya usalama vilikuwa pembeni ya umati, wakiwa na bunduki begani wakiweka usalama wakati sherehe hizo zikiendelea.

Sheikh Abati Abba Nur, mwanachuoni wa Kiislamu, aliwahimiza Waislamu kumcha Mungu, huku akisisitiza umuhimu wa sherehe hizo.

Baadhi ya waliokua katika sherehe hizo walisema sikukuu hiyo ina maana ya kipekee binafsi.

"Watu wanaanza kutambua umuhimu wa siku hii," alisema Fadumo Abdulkadir, aliyeshiriki katika hafla hiyo.

Sherehe za Maulidi nchini Somalia hapo awali zilifanyika kwa siri kutokana na vitisho kutoka kwa kundi la ugaidi la Al Shabaab hadi pale walipofurushwa kutoka Mogadishu zaidi ya miaka kumi iliyopita.

Tangu wakati huo, mikusanyiko hiyo imerejea na kuendelea kukua kila mwaka kutokana na kuimarika kwa usalama nchini.

Wakati nchi nyingi zenye Waislamu wengi huadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Mtume kama sikukuu ya kitaifa, nchi nyingine hazifanyi hivyo.

 

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us