Mwezi Agosti mwaka 2025, utabakia kuwa wa kipekee katika safari ya kisiasa ya Luhaga Joelson Mpina.
Mpina alijiunga na chama cha upinzania cha ACT Wazalendo mwanzoni mwa mwezi Agosti baada ya ‘kutoswa’ na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika hatua za kura za maoni, akisaka jimbo la Kisesa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Pengine wanaomfuatilia kwa makini hawakushangazwa kufuatia misimamo yake ya wazi, huku akitofautiana waziwazi na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ndiye mwenyekiti wa CCM.
Mpina hakufurahishwa na hatua ya ‘kutelekeza’ jimbo lake kwenye masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Historia ya Mpina
Luhaga Joelson Mpina alizaliwa Mei 5, 1975.
Ana Shahada ya Kwanza ya Uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe na Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde.
Alichaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Kisesa mwaka 2005, aliendelea na nafasi hiyo kwa awamu mfululizo—2010, 2015, na 2020.
Aliteuliwa kuongoza wizara mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa kama Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kati ya 2015 na 2017, Waziri wa Mifugo na Uvuvi kati ya Oktoba 2017 na Juni 2020 chini ya Serikali ya Rais Magufuli.
Mwanasiasa jasiri
Mpina haraka alijizolea sifa ya kuwa mmoja wa wabunge wa CCM wenye sauti kubwa na wasio na woga, bila kukwepa kupinga maamuzi ya serikali au kudai uwazi.
Aliongoza tume mbalimbali zilizochunguza miradi na mikataba tata nchini Tanzania, ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Tegeta (IPTL), Songas, na michakato ya manunuzi.
Aliwahi kumshitaki mwanasheria mkuu wa serikali na mawaziri wa kilimo na fedha—kuhusu vibali tata vya kuagiza sukari, akiangazia matumizi mabaya ya mamlaka ya serikali.
Itakumbukwa kuwa, aliwahi kusimamishwa kuhudhuria vikao 15 vya bunge kwa kosa la kutoheshimu ofisi ya spika, wakati wa sakata la uagizaji sukari.
Kuitosa CCM na kujiunga upinzani
Mnamo Julai 2025, Mpina aliondolewa katika orodha ya wagombea ubunge wa CCM bila kutarajiwa, jambo ambalo linatafsiriwa na wengi kama kulipiza kisasi kwa msimamo wake wa kujitokeza na ukosoaji wa uongozi wa chama.
Mapema Agosti, alihama rasmi na kujiunga na ACT-Wazalendo, akipokea kadi ya uanachama na fomu ya kugombea urais—ikiashiria mhimili mkubwa katika mwelekeo wake wa kisiasa.
Mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo ulimpitisha Mpina kama mgombea rasmi wa Urais kwa tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Vizingiti vya kisheria
Mpina aliielezea uamuzi wake kama wajibu wake wa uokoaji kwa chama alichodai kuwa kimekengeuka kutoka kwa misingi yake. Aliishutumu CCM kwa kutekwa na wasomi, kupoteza mawasiliano na mapambano ya chinichini, na kusaliti ahadi yake ya kuwainua maskini.
Hata hivyo, mmoja wa maofisa wa chama hicho aitwaye Monalisa Joseph Ndala, aliwasilisha malalamiko yake akidai Mpina alikiuka kanuni za chama—hasa kwa kujiunga na chama akiwa amechelewa kwa hiyo hastahili uteuzi wa kugombea Urais.
Hatimaye, Msajili wa Vyama vya Siasa alimzuia kugombea, akitaja ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa msingi. Uamuzi huo ulilaaniwa vikali na uongozi wa chama kuwa ulichochewa kisiasa.
Mchango wake kisiasa
Safari ya Mpina—kutoka kuongoza wizara mbalimbali ndani ya Tanzania hadi kuibukia kwenye kambi ya upinzani inaashiria mabadiliko ya taswira ya demokrasia nchini humo.
Hata hivyo, zikiwa zimesalia wiki saba kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, bado hatma ya ACT Wazalendo kwenye uchaguzi huo ni ipi.