Mkutano wa Pili wa Hali ya Hewa Afrika ulianzishwa Jumatatu huko Addis Ababa huku kukiwa na wito wa kubadilisha maneno kuwa vitendo kutoka kwa viongozi.
Walisisitiza kuonesha Afrika sio tu kama muathiriwa wa mabadiliko ya hali ya hewa, bali kama mtendaji wa suluhisho na uchumi mpya wa hali ya hewa duniani.
Akianzisha mkutano huo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, aliwahimiza washirika badala ya kuisaidia Afirka kwa misaada, badala yake wawekeze katika bara hilo.
“Mara nyingi matamshi ya Afrika katika mikutano ya hali ya hewa huanza na kile ambacho hatuna: fedha, teknolojia, na muda. Hebu tuanze badala yake na kile tulicho nacho,” Abiy alisema, akionyesha idadi kubwa ya vijana wa Afrika, ardhi kubwa inayofaa kilimo, na mkoa unaokua kwa kasi zaidi wa umeme wa jua duniani.
Alibainisha Mpango wa Urithi wa Kijani wa Ethiopia, ambao umeweka zaidi ya miti bilioni 48, na uzinduzi wa Bwawa Kubwa la Ethiopia (Grand Ethiopian Renaissance Dam) unaotarajiwa kuzalisha megawati 5,000 za umeme.
“Hatujakuja hapa kujadiliana juu ya kuishi kwetu. Tuko hapa kubuni uchumi mpya wa hali ya hewa duniani,” Abiy alisema. “Afrika itashinda pale ardhi yake itakapokuwa sawa, mito yetu itakapokuwa safi, na hewa yetu ikiwa safi.”
Pia alipendekeza mpango wa ubunifu wa hali ya hewa wa Afrika, ushirikiano wa dola bilioni 50 kwa mwaka wa kutoa suluhisho 1,000 za hali ya hewa Afrika ifikapo 2030 katika sekta za nishati, kilimo, maji, usafiri, na ustahimilivu.
Alitangaza rasmi Ethiopia kuomba kuwa mwenyeji wa mkutano wa COP32 mwaka 2027, akitoa Addis Ababa kama mji mkuu wa hali ya hewa Afrika.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, alisisitiza usawa katika ufadhili wa kimataifa.
“Tume ya Umoja wa Afrika inaamini kwa dhati kwamba ufadhili wa hali ya hewa lazima uwe wa haki, mkubwa, na unaotarajiwa,” Youssouf alisema.
“Udhaifu wa nchi zetu kama wanachama, uliozidiwa na mabadiliko ya hali ya hewa, mzigo wa madeni, na ukosefu wa usawa katika mfumo wa kifedha wa kimataifa, lazima ushughulikiwe kwa njia ya haki katika masuala ya hali ya hewa na ushirikiano wa kweli.”
Rais wa Kenya, William Ruto, ambaye alikuwa msemaji kwenye mkutano wa kwanza wa Hali ya Hewa Afrika, Nairobi, mwaka 2023, aliisifu Ethiopia kwa kuendeleza haraka maendeleo hayo.
“Hakuna taifa linaloweza kutatua janga hili peke yake. Ushirikiano jasiri, mshikamano na endelevu pekee ndilo linaloweza kuzuia majanga ya hali ya hewa.”
Mkutano wa siku tatu, uliofanyika chini ya kaulimbiu “Kukuza Haraka Suluhisho za Hali ya Hewa Duniani: Ufadhili kwa Maendeleo Endelevu na Yenye Mazingira Safi Afrika,” ulijumuisha sherehe ya kupanda miti katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Addis Ababa, ambapo viongozi wa nchi waliahidi mshikamano na kujitolea katika kurejesha mifumo ya ikolojia.