Alassane Ouattara wa Cote d’Ivoire
Alassane Ouattara wa Cote d’Ivoire
Alassane Dramane Ouattara ni Rais wa Cote d’Ivoire ambaye amekuwa rais wa taifa hilo la Afrika Magharibi tangu mwaka 2010 na hivi majuzi ametangaza kugombea tena katika uchaguzi wa Urais wa mwezi Oktoba.
5 Agosti 2025

Ouattara alizaliwa tarehe mosi Januari 1942 na kwa sasa ana umri wa miaka 83. Kitaaluma yeye ni mwanauchumi.

Amefanya kazi na Shirika la Fedha Duniani IMF na baadaye Benki Kuu ya Afrika Magharibi kati ya miaka ya sitini hadi mwishoni mwa miaka ya themanini.

 Alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Cote d’Ivoire 1990 wakati huo rais akiwa Felix Houphouet-Boigny.

Baada ya rais Houphouet-Boigny kufariki dunia mwaka 1993 kukawa na mvutano wa nani atamrithi huku Ouattara akitofautiana na aliyekuwa rais wa bunge la nchi hiyo Henri Konan Bedie ambaye kikatiba ndiye anayeruhusiwa kurithi uongozi.

Ouattara alijiuzulu na kurudi kwenye kazi yake ya IMF na kuhudumu kama Naibu Mkurugenzi Mkuu hadi 1999.

Jeshi likafanya mapinduzi lakini Ouattara hakuruhusiwa kusimama uchaguzi wa 2000 kutokana na kura ya maamuzi iliyotaka mgombea wa urais awe na wazazi wote wawili wenye asili ya Cote d’Ivoire.

 Kukawa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na hakugombea urais hadi 2010 na Tume ya Uchaguzi ikamtangaza kuwa mshindi, huku rais Laurent Gbagbo akitangaza hafla tofauti ya uapisho.

Baada ya vuta nikuvute Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa ukamtambua Alassane Ouattara kama rais halali wa nchi hiyo.

Uchaguzi uliofuata wa 2015 alishinda kwa asilimia 84 ya kura zilizopigwa.

 Mwaka 2020, Ouattara alitangaza kuwa hatogombea tena na kumuunga mkono Waziri Mkuu Amadou Gon Coulibaly wa chama chake cha RDR. Coulibaly alifariki dunia kabla uchaguzi, na Ouattara akarudi tena uwanjani kupeperusha bendera.

 Kwa sehemu kubwa upinzani ulisusia uchaguzi huo na akashinda kwa asilimia 95.31.

Mwezi Juni mwaka huu chama chake cha RDR kikamteua tena kuwa mgombea wake na yeye mwenyewe akathibitisha mwezi uliopita kuwa atakuwepo kwenye kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi wa Oktoba.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us