Ijue tofauti ya michuano ya CHAN 2024 na ile ya AFCON
AFRIKA
2 dk kusoma
Ijue tofauti ya michuano ya CHAN 2024 na ile ya AFCONMichuano ya CHAN 2024, inaandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.
Clement Mzize aliifungia Tanzania mabao mawili katika ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Madagascar./Picha:Wengine

Michuano ya CHAN 2024 inaendelea kurindima katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Hadi kufikia sasa, zipo timu zilizofurahia matokeo yao kwenye hatua za makundi, na zipo zile ambazo bado hazijafahamu hatma yao, ndani ya mashindano hayo maalumu kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani barani Afrika.

Je, unafahamu tofauti ya michuano ya CHAN na ile Kombe la Mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON?

Ipo hivi.

Wakati michuano ya CHAN ikihusisha wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani, michuano ya AFCON hukutanisha wachezaji wa ligi za ndani na nje ya nchi wanazochezea.

 Ngoja nikupe mfano huu.

Kiungo wa Kenya Mohammed Bajaber, alikuwa ni sehemu ya Harambee Stars ambacho kinashiriki CHAN 2024 akiwa na timu ya Kenya Police.

Hata hivyo, ameshindwa kushiriki kwenye michuano ya CHAN, baada ya kusajiliwa na Simba Sports Club ya Tanzania.

Vivyo hivyo kwa Mbwana Samatta na Simon Msuva, ambao wanachezea nje ya Tanzania.

 Ila wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani na wale wanaoshiriki ligi za nje, hukutana pamoja kwenye timu zao za taifa, wakati wa michuano ya AFCON.

Wakati michuano ya CHAN ikiwa imeanza mwaka 2009, mashindano ya AFCON yalianza mwaka 1957.

 Vile vile, michuano ya AFCON inatambulika kama mashindano makubwa na yenye hadhi ya kipekee barani Afrika, wakati michuano ya CHAN yanachukuliwa kama jukwaa la kukuza vipaji vya ndani tu.

 Wakati mashindano ya AFCON yakipata msukumo na mguso wa kimataifa, mashindano ya CHAN yamejizoelea umaarufu tu ndani ya bara la Afrika.

Unakumbuka kauli za kocha Jose Mourinho na beki wa zamani wa Liverpool Jamie Carragher?

“Umuhimu wa michuano ya AFCON unazidi kuonekana siku hadi siku. Binafsi, napenda zaidi kuangalia michuano ya AFCON kutokana na uwezo wake wa kuzalisha wachezaji wenye vipaji,” aliwahi kunukuliwa akisema kocha huyo wa klabu ya Fenerbahce inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Uturuki.

 Hali ilikuwa tofauti kwa Carragher, ambaye alikosolewa vikali na wapenda soka barani Afrika, kwa kitendo cha ‘kudogosha’ na ‘kuidharau’ michuano ya AFCON.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us