Zimbabwe imerejesha marufuku ya uagizaji wa mahindi ili kuwasaidia wakulima wa ndani, baada ya mavuno mazuri mwaka huu ambayo yamewezesha nchi hiyo kuzalisha mahindi ya kutosha kwa ajili ya viwanda vyake vya kusaga nafaka, afisa mwandamizi wa wizara ya kilimo alisema Jumatatu.
Mvua za kutosha zimeongeza uzalishaji na kubadili hali mbaya ya mwaka uliopita ambapo ukame uliosababishwa na El Nino ulilazimisha nchi kutegemea uagizaji wa mahindi, yakiwemo yale yaliyobadilishwa vinasaba.
"Tunakagua hali kila siku. Lazima tulinde ununuzi wa ndani kutoka kwa wakulima wetu wa ndani," alisema Obert Jiri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, alipoongea na Reuters.
Zimbabwe, ambayo hutumia takriban tani milioni 1.8 za mahindi kila mwaka, iliona uzalishaji wake ukishuka hadi takriban tani 800,000 katika mwaka wa 2023/24 kutoka tani milioni 2.3 miaka miwili iliyopita.
Hali hiyo ya upungufu ililazimisha serikali ya kusini mwa Afrika kuondoa kwa muda vikwazo vya uagizaji ili kupunguza uhaba wa chakula.
Jiri alisema kuwa mafanikio ya mwaka huu, pamoja na programu za msaada wa serikali kama mpango wa wakulima wadogo wa Pfumvudza, yameiwezesha nchi kuwa na akiba ya kutosha.
Mchambuzi huru Paul Chidziva anasema kuwa sekta ya kilimo ya Zimbabwe – ambayo inaajiri takriban asilimia 70 ya watu – bado iko hatarini kutokana na ukame na matukio mengine ya hali mbaya ya hewa yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi.
Serikali inahimiza kilimo cha mazao yanayostahimili ukame kama vile mtama na ulezi. Jiri alisema kuwa ziada ya sasa inatoa fursa adimu ya kuimarisha usalama wa chakula na kupunguza utegemezi wa uagizaji.
Zimbabwe ilitumia dola milioni 300 kuagiza mahindi mwaka 2020 baada ya ukame wa mfululizo kuacha zaidi ya nusu ya idadi ya watu wakihitaji msaada wa chakula.