Wachezaji na benchi la ufundi la timu ya taifa ya Kenya, ‘Harambee Stars’ watalazimika kuweka kibindoni Shilingi 500,000 tu za Kenya, na sio kitita cha Shilingi 1,000,000 kama walivyoahidiwa na Rais William Ruto, baada ya kutoshana nguvu na Angola, katika mchezo wa pili wa Kundi A wa michuano ya CHAN 2024, uliofanyika Agosti 7, 2025 katika uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi.
Angola, maarufu kama ‘Paa Weusi’ ndio walikuwa wa kwanza kuliona lango la wapinzani, kupitia bao la dakika ya 7 ya mchezo, lililowekwa kimiani na Jó Paciência.
Hata hivyo, ‘Harambee Stars’ walicharuka na kusawazisha dakika tano baadaye, kupitia kwa nyota wao, Austin Odhiambo.
Kenya ilipata pigo katika dakika ya 21 ya mchezo baada ya Marvin Omondi kuoneshwa kadi nyekudu baada ya kumfanyia madhambi mshambuliaji wa Angola, na hivyo kulazimika kucheza pungufu hadi mwisho wa mchezo.
Kitakwimu, Angola ndio waliomiliki mpira zaidi, wakiwa na asilimia 71 dhidi ya 21 za Kenya.
Kenya walikuwa na asilimia moja tu ya mashuti yaliyolenga goli la wapinzani wao, huku ‘Paa Weusi’ wakiwa na asilimia saba.
Kama si maamuzi ya Video ya Kumsaidia Refa (VIKURE) katika dakika za salama za mchezo, basi tungekuwa tunazungumza mengine, baada ya bao la Angola lililofungwa na Kaporal kukataliwa na mwamuzi kwa kuwa mfungaji alikuwa ameotea.