Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema kuwa nchi yake ni mdhamini wa usalama, amani na ustawi wa Wakurdi, kama ilivyo kwa ndugu zetu nchini Syria.
Matamshi hayo ya Erdogan yametolewa Jumanne, wakati wa hotuba yake ya kuadhimisha miaka 954 ya ushindi wa Malazgirt, katika jimbo la Mus, Uturuki.
“Wale watakaoelewana Ankara na Damascus ndio watakaoshinda,” alisema Erdogan katika hotuba hiyo.
Amesisitiza kuwa dira ya ‘Karne ya Uturuki’ inalenga kuijenga Uturuki iliyo kubwa, yenye nguvu na isiyo na ugaidi, na kwamba mafanikio hayo yataenea katika ukanda mzima kupitia juhudi za pamoja.
Ameongeza kuwa licha ya vikwazo, vizingiti na hujuma mbalimbali, Uturuki itaendelea kujitahidi kujijenga kama taifa lenye nguvu, linalojumuisha watu milioni 86 waliounganishwa na historia, utamaduni, ustaarabu wa pamoja na imani za pamoja.
“Kama Waturuki, Waarabu na Wakurdi, tutaishi pamoja bega kwa bega katika ardhi hii hadi mwisho,” alisema Erdogan.
Kauli hiyo imekuja wiki chache baada ya Bunge la Uturuki kuanzisha kamati ya ngazi ya juu inayolenga kuandaa njia ya kisheria kuelekea ‘Uturuki isiyo na ugaidi,’ hatua ambayo viongozi wa Uturuki wameieleza kuwa ni mgeuko wa kihistoria katika harakati za kuleta amani ukanda mzima.
Kamati hiyo, iliyopewa jina la Kamati ya Mshikamano wa Kitaifa, Udugu na Demokrasia, ilizinduliwa rasmi tarehe 5 Agosti.
Kamati hiyo inalenga kuwa jukwaa la mazungumzo kati ya Waturuki na Wakurdi, na kutatua tofauti zilizoko kupitia bunge.
“Udugu kati ya Waturuki na Wakurdi ni msingi wa jiografia yetu,” alisema Spika wa Bunge la Uturuki, Numan Kurtulmus, wakati wa hafla ya uzinduzi wa kamati hiyo.
“Hatua hii ni suala la uhai wa kitaifa, linalohusu mustakabali wa pamoja wa Waturuki, Wakurdi na raia kutoka makundi yote ya kijamii,” aliongeza.
Viongozi wanasema kamati hiyo itakuwa na jukumu la kutoa mapendekezo ya mageuzi, kuandaa miswada ya sheria na kuwaelimisha wananchi kuhusu maendeleo ya kazi zake, hadi mwisho wa mwaka 2025.
Onyo la kikanda
Mnamo Machi 10, ofisi ya Rais nchini Syria ilitangaza kutiwa saini kwa makubaliano ya kuingiza vikosi vya SDF (Syrian Democratic Forces) katika taasisi za serikali, hatua iliyolenga kuthibitisha umoja wa ardhi ya Syria na kupinga jaribio lolote la kuigawanya.
Hata hivyo, miezi kadhaa baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Rais wa Syria, Ahmad al Sharaa, aliikosoa SDF kwa kile alichokieleza kuwa ni kutokuwepo kwa ulinganifu kati ya maneno na vitendo kuhusu utekelezaji wa makubaliano hayo.
Mnamo Julai, magaidi 30 wa PKK walichoma silaha zao kaskazini mwa Iraq, hatua ambayo Ankara ilieleza kuwa ni mwanzo wa kuvunjwa kwa kundi hilo.
Tukio hilo lilichukuliwa kama mojawapo ya ishara kubwa katika kampeni ya muda mrefu ya ugaidi dhidi ya Uturuki kutoka kwa PKK, kundi linalotambuliwa kuwa la kigaidi na Ankara, Marekani na Umoja wa Ulaya.
SDF inatajwa kuwa inatawaliwa na kundi la kigaidi la YPG, ambalo ni tawi la PKK nchini Syria.
Mnamo Agosti 13, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, alilitaka kundi la YPG kusitisha mara moja vitendo vyake vya kutishia Uturuki na ukanda mzima.
“Wito wangu kwa YPG ni kwamba waondoe mara moja vitisho kwa Uturuki na ukanda huu, pamoja na magaidi waliowakusanya kutoka maeneo mbalimbali duniani,” alisema Fidan wakati wa mkutano wa pamoja na mwenzake wa Syria.