ULIMWENGU
5 dk kusoma
Subira ya Putin, hila ya Trump huko Alaska na mgogoro wa Ukraine
Hivi karibuni, Urusi ilianzisha tena vita vilivyokuwa kwa zaidi ya miongo miwili. Huku Donald Trump akitarajiwa kukutana na Vladimir Putin huko Alaska, swali kuu ni iwapo pande zote mbili ziko tayari kuachana na baadhi ya matakwa.
Subira ya Putin, hila ya Trump huko Alaska na mgogoro wa Ukraine
Mazungumzo ya Alaska kati ya Vladimir Putin na Donald Trump yatakuwa na tija? / AP
13 Agosti 2025

Na Talha Yavuz

Kabla ya raundi ya pili ya mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine mwezi Mei, mpatanishi mkuu wa Urusi, Vladimir Medinsky, aliangazia historia ya karne ya 18 kwa kulinganisha historia. Katika tamko lake, alirejelea Vita Vikuu vya Kaskazini kati ya Milki ya Urusi na Uswidi – vita vilivyochukua miaka 21.

Ujumbe wake ulikuwa wazi: Urusi iko tayari kupigania Ukraine kwa muda wowote utakaohitajika.

Kauli hiyo, iliyotolewa miezi michache tu iliyopita, sasa inasomeka kwa mtazamo tofauti. Mapambano bado yanaendelea uwanjani, huku mazungumzo ya upatinishi yamekwama. Na sasa, katika mabadiliko yasiyotabirika wakati vita vilipoanza, hatua inayofuata ya mgogoro huu wa muda mrefu haitochukuliwa Kiev au Moskow, bali huko Anchorage, Alaska.

Ijumaa hii, Donald Trump atakutana na Vladimir Putin huko Alaska. Inatarajiwa kuwa Ukraine ndiyo itakayokuwa ajenda kuu, ingawa bado haijajulikana iwapo Rais Volodymyr Zelenskyy atahudhuria.

Putin anaripotiwa kubeba pendekezo la kusitisha mapigano: kusitisha uhasama kwa masharti ya Urusi kudhibiti maeneo ya mashariki mwa Ukraine. Zelenskyy tayari amekataa masharti hayo, akisisitiza kuwa hatakubali kutoa hata kipande cha ardhi katika makubaliano yoyote ya amani.

Mkutano huo unaweza kutoa msukumo mpya kwa raundi ya nne ya mazungumzo inayotarajiwa kufanyika Istanbul, ingawa tarehe bado haijatangazwa.

Hadi sasa, mazungumzo hayo yamekuwa ya manufaa zaidi katika kudumisha mawasiliano na kuratibu hatua za kujenga imani kama vile kubadilishana wafungwa.

Lakini ni vigumu kufikiria mafanikio makubwa yatapatikana huko Anchorage. Mkutano huu utakuwa mtihani wa kuonesha iwapo kuna upande wowote unaoweza – au hata una nia – ya kurudi nyuma kutoka kwenye misimamo mikali ambayo imefanya maendeleo ya mazungumzo kuwa jambo lisilowezekana.

Madai makubwa, matokeo madogo

Hatua tatu za mazungumzo tayari zimefanyika bila mafanikio ya maana.

Mapendekezo ya Ukraine yanasisitiza haki ya kujiunga na NATO na kukataa masharti yoyote yanayozuia majeshi ya washirika kuingia Ukraine – jambo ambalo Moscow linaona kama tishio kwake. Hili ndilo lilikuwa miongoni mwa sababu kuu ambazo Kremlin ilitoa kuhalalisha uvamizi wake.

Mapendekezo ya Urusi pia ni magumu: kuitisha uchaguzi wa rais nchini Ukraine ndani ya siku 100 baada ya sheria ya kijeshi kuondolewa, pamoja na kutambuliwa kimataifa kwa Crimea na maeneo manne inayoamini kuwa imeyatawala – Donetsk, Luhansk, Kherson, na Zaporizhzhia.

Ukraine bado inadhibiti sehemu kubwa ya maeneo hayo matatu (isipokuwa Luhansk), na hivyo kufanya jambo la kuyaachia kuwa sumu kisiasa kwa serikali ya Kiev.

Hii imeleta kile ambacho kinaweza kuitwa mkwamo wa kimakusudi – hakuna upande unaomba kile ambacho upande mwingine anaweza kutoa.

Gharama zilizofichika kwa Moscow

Uwanjani, Urusi inaendelea kusonga polepole, ikizidi kujitanua katika Donetsk. Mji wa Pokrovsk, ambao ni wa kimkakati kwa Ukraine, huenda ukadhibitiwa na Urusi hivi karibuni. Lakini mafanikio haya yanakuja kwa gharama kubwa kwa Moscow.

Licha ya mafanikio haya ya ardhini, vita vya Ukraine vimeilazimisha Urusi kupunguza ushawishi wake kwingineko.

Huko Syria, ambako Moscow imewekeza sana tangu 2015 ili kumuunga mkono Bashar al Assad na kulinda bandari yake pekee ya maji ya joto, majeshi ya Urusi sasa yamepungua hadi kuwa vikosi vidogo tu katika vituo vya Tartus na Hmeymim, vikisubiri hatma yao chini ya washirika wapya wa kikanda.

Uwezo wa Kremlin kushughulikia masuala mengine pia umepungua. Imeshindwa hata kujibu kwa nguvu mvutano unaozidi kuongezeka na majirani wake kama Azerbaijan, kufuatia matukio kama kuangushwa kwa ndege na kukamatwa kwa wafanyakazi wa shirika la Sputnik mjini Baku.

Kisha kuna suala la Iran: kama Moscow haingekuwa imezama kwenye vita vya Ukraine, huenda ingechukua hatua zaidi ya maneno dhidi ya mashambulizi ya Israel na Marekani kwa mshirika wake huyo muhimu.

Kuhusu matamshi ya Putin kuhusu kurejesha hadhi ya Urusi, vita hivi vimeonyesha kinyume chake.

Nguvu za ndani zilizoko mstari wa mbele Ukraine

Nguvu za Ukraine hazipo tu Donbas.

Ndani ya nchi, Rais Zelenskyy anakumbwa na misukosuko ya kisiasa. Mwezi uliopita, maandamano ya wananchi yalimlazimu kufuta sheria iliyokuwa inapanua mamlaka ya Mwanasheria Mkuu juu ya Shirika la Kitaifa la Kupambana na Rushwa (NABU).

Katika utafiti wa mwaka 2024 uliofanywa na taasisi ya Rating Group, wananchi wa Ukraine waliorodhesha rushwa kama tishio kubwa zaidi kwa maendeleo ya taifa hilo kuliko hata uvamizi wa Urusi.

Zelenskyy, ambaye alichaguliwa kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura, katika siku zake za kuiga tamthilia, aliiga kama mtu anayepambana na rushwa, sasa anaungwa mkono na asilimia 63 tu. Mkuu wa zamani wa majeshi, Valeriy Zaluzhny – ambaye alifutwa kazi mwaka jana – ndiye sasa anayeongoza kwa umaarufu kwa asilimia 73.

Sheria ya kijeshi bado ipo tangu vita kuanza mwaka 2022, na uchaguzi haujafanyika tangu wakati huo. Taifa hilo lingekuwa limeenda kwenye uchaguzi mwezi Machi 2024.

Trump naye ameongeza vurugu lake la kipekee, akiwahi kuhoji uhalali wa Zelenskyy wakati wa mvutano wa biashara ya madini adimu, kabla ya kurudi nyuma mara baada ya kupata makubaliano aliyoyataka. 

Kwa changamoto hizi za ndani na shinikizo za nje kwa pande zote mbili, si ajabu kwamba mafanikio ya kweli yanabaki kuwa mbali. Iwapo mkutano wa wiki hii huko Alaska utazaa matunda yoyote, basi huenda yakawa ya ishara tu, si ya maamuzi.

Vita bado ni mchuano wa nia za kisiasa, badala ya kutafuta mwafaka.

Na kama historia inavyotufundisha, vita vinavyoanza na malengo yasiyoyumbika huwa na tabia ya kudumu. Katika Vita Kuu ya Kaskazini, kila upande ulikuwa na hakika kuwa unaweza kumshinda mwenzake kwa subira. Na wote walikuwa sahihi – mpaka pale uchovu na mabadiliko ya miungano vilipobadili mchezo miongo miwili baadaye.

Ikiwa Urusi au Ukraine hawapo tayari kuachia misimamo yao mikali, vita vya sasa huenda visidumu miaka 21 kama vile vya Uswidi – lakini vitadumu zaidi ya vile ambavyo yeyote atakayekuwepo Alaska wiki hii yuko tayari kukiri.

CHANZO:TRT World
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us