Rais wa Urusi Vladimir Putin ameishukuru Uturuki kwa juhudi zake za upatanishi katika mzozo wa Ukraine na kusema kuwa ana imani kwamba Ankara itaendelea kuwa na "nafasi maalum" katika kutafuta suluhu. Rais Putin aliyasema hayo alipokutana na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kando ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) katika mji wa bandari wa Tianjin wa China.
Putin alisema tangu Mei, duru tatu za mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Urusi na Ukraine yamefanyika mjini Istanbul.
Kulingana naye, mazungumzo hayo yaliruhusu pande hizo kusonga mbele katika masuala kadhaa ya kibinadamu. Alisisitiza kwamba ushiriki wa Ankara umekuwa muhimu katika kuunda nafasi ya mazungumzo, akielezea mchango wa Uturuki kama "muhimu" na "unaohitajika."
Kiongozi huyo wa Urusi pia alisema yeye na Erdogan walijadili masuala kadhaa ya kikanda, ikiwa ni pamoja na Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na eneo la Kaukasi. Alisisitiza kwamba ushirikiano na Uturuki katika maeneo haya ni "imara, thabiti, muhimu na ya kuaminiana."
Putin alidokeza kuwa mazungumza ya mara kwa mara katika ngazi ya urais yanasaidia kuendeleza kile alichokiita mazungumzo ya kujenga na yenye heshima, ambayo alisema yanaendana na kanuni za ujirani mwema.
Putin pia aliangazia kuendelea kukua kwa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Alisema biashara baina ya nchi hizo mbili ilipanda kwa asilimia 6.6 mwaka jana na kuongeza asilimia nyingine tatu katika nusu ya kwanza ya 2025. Makampuni ya Kirusi, alibainisha, yanafanya kazi katika viwanda vya madini na magari ya Uturuki, wakati makampuni ya Kituruki yanadumisha uwepo unaoonekana nchini Urusi katika uhandisi wa mitambo, mbao na vyuma.
Kazi ya tume ya serikali, ambayo ilikutana hivi karibuni huko Moscow mnamo Juni, pia ilitajwa kuwa kichocheo cha ushirikiano wa kiuchumi.
Ushirikiano wa nishati ulielezewa na Putin kama "mkakati wa kweli." Alisema uwasilishaji wa gesi asilia kupitia mabomba ya ‘Blue Stream na Turkish Stream’ unasalia bila ya kusitishwa na kusisitiza kuwa Urusi inaendelea kuwa mmoja wa wasambazaji wakuu wa Uturuki.
Aliangazia zaidi kinu cha nyuklia cha Akkuyu, ambacho kwa sasa kinajengwa na Rosatom ya Urusi, na kukiita mradi mkuu wa uhusiano wa nchi mbili ambao unaashiria hali ya muda mrefu ya ushirikiano. Katika muda mfupi kabla ya mazungumzo rasmi, Kremlin ilitoa picha zinazoonyesha wajumbe wa Urusi na Uturuki wakisalimiana kwa furaha.
Mkuu wa Rosatom Alexey Likhachev na Waziri wa Nishati wa Urusi Sergey Tsivilev walipeana mikono na kukumbatiana na wenzao wa Uturuki akiwemo Waziri wa Nishati Alparslan Bayraktar.
Putin pia aliashiria umuhimu wa uaminifu wa kisiasa kati ya Moscow na Ankara, akibainisha kuwa ushirikiano wao umejizatiti zaidi kutoka masuala ya mataifa mawili hadi masuala ya kikanda na kimataifa.
Alisema kuwa pande zote mbili zinaona thamani ya kuoanisha mbinu katika kanda kama vile Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, ambako maslahi yao mara nyingi yanaingiliana.