Uwasilishaji wa taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa Rais ni tukio la kikatiba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 143 (4).
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kumekuwa na ongezeko la ufanisi katika matumizi ya rasilimali za Serikali katika miaka ya hivi karibuni hali inayoashiria mafanikio katika kukuza uwazi, uwajibikaji na utawala bora.
Rais Samia amesema hayo katika hafla ya kupokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2023-2024 pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iliyofanyika Ikulu Machi 27, 2025.
Rais Dkt. Samia amesema pamoja na mapungufu yaliyotajwa na ripoti hiyo, ambapo baadhi yamekuwepo kwa miaka mingi, lakini amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la ufanisi wa matumizi ya rasilimali za Serikali.
“Niipongeze timu nzima ya CAG kwa kazi waliyoifanya wamekagua hesabu za fedha, lakini wamekagua ufanisi wa miradi na Taasisi mbalimbali. Wamefanya uchunguzi na kaguzi za mifumo ya TEHAMA kama zinafaya kazi inayotakiwa. Ukaguzi uliofanywa unatupa taswira ya matokeo ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia taasisi za umma” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameshukuru jitihada zinazofanywa na Taasisi za umma na kuzitaka zitumie vizuri rasilimali za Serikali na kufuata taratibu zinazotakiwa za matumizi ya rasilimali hizo.
Wakati huo huo, Rais Samia amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Francis Chalamila ambapo amebainisha kuwa Taarifa imeonyesha kuongezeka kwa ufanisi ndani ya TAKUKURU.
Ripoti hizo za CAG licha ya kuonyesha mafanikio katika usimamizi wa fedha za umma, lakini pia, zimeendelea kuonyesha changamoto zilizopo katika baadhi ya mashirika ya umma ikiwemo ile ya kuendelea kupata hasara.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameweka bayana kuwa Serikali yake ipo tayari kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa ndani ya taarifa hizo mbili, kwa nia ya kujenga utawala bora ndani ya nchi.
“Sisi upande wa Serikali tupo tayari kuendelea kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa ndani ya taarifa hizi mbili, tutasikiliza vizuri, tutafuatilia vizuri mjadala wa Bunge kwenye taarifa ya CAG lakini pia kwa taarifa ya TAKUKURU tutafanyia kazi vizuri yaliyoelezwa ili tujenge utawala bora ndani ya Nchi yetu,” amesema Rais Samia.
Uwasilishaji wa taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa Rais ni tukio la kikatiba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 143 (4).