Faure Essozimna Gnassingbé alizaliwa 1966 katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.Alipata masomo yake mjini Lome, na baadaye nchini Marekani na Ufaransa.
Amekuwa Rais wa awamu ya nne wa taifa hilo ambapo alishika hatamu baada ya kifo cha baba yake Gnassingbé Eyadéma mwaka 2005.
Baba yake alikuwa rais wa awamu ya tatu kuanzia mwaka 1967 hadi 2005, uongozi uliodumu kwa takriban miongo minne.
Kuingia madarakani kwa Faure Gnassingbe kuligubikwa na utata huku nafasi hiyo kikatiba ilitakiwa kwenda kwa rais wa bunge wakati huo akiwa ni Fambaré Ouattara
Natchaba.
Faure Gnassingbe amewahi kuhudumu katika nafasi za uwaziri katika serikali ya baba yake.
Alishinda uchaguzi wa 2010, na mwaka 2015 akapewa mitano tena kwa ushindi wa asilimia 59 kulingana na matokeo rasmi.
Mwaka 2020 ushindi ukawa mkubwa zaidi kwa zaidi ya asilimia 70.
Mabadiliko ya Katiba ya 2024 yalihamisha jukumu la mamlaka kutoka kwa Rais hadi kwa Waziri Mkuu na mwezi Mei 2025 Gnassingbe akawa Waziri Mkuu.
Upinzani ulishutumu hatua hiyo ukisema kuwa ulikuwa na maana ya kumuweka Faure Gnassingbe madarakani maisha yake yote.
Pamoja na kuwa uchaguzi wa urais ulifanyika mwaka huu mwezi Mei, kulikuwa na mgombea mmoja pekee Jean-Lucien Savi de Tové, ambae alipita bila kupingwa, ingawa nafasi yake haina mamlaka kamili.
Madaraka kamili ya kikatiba ya taifa hilo la Afrika Magharibi lenye watu takriban milioni 9 yanabaki mikononi mwa Waziri Mkuu ambaye kwa sasa ni Faure Essozimna Gnassingbé.