Chama Cha Demokrasia na Maendeleo cha nchini Tanzania (CHADEMA) kimeiandikia barua ya malalamiko, kamati ya maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), ikiilalamikia klabu ya soka ya Young Africans, kwa madai ya kujihusisha na siasa nchini humo.
Katika barua yake ya Agosti 15, 2025, chama hicho cha upinzani kimeitaka FIFA kuichukulia hatua klabu ya Young Africans kwa madai ya ukiukwaji wa kanuni za michezo ambazo zinaweka msisitizo kwenye ‘uhuru’ wa kutokuegemea upande wowote.
Katika harambee iliyofanyika Agosti 12 jijini Dar es Salaam, klabu ya Young Africans ilitoa kiasi cha milioni 100 kuisadia CCM katika kampeni zake, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Hali kadhalika, katika harambee hiyo hiyo, mdhamini na mfadhili wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohamed alitoa shilingi Bilioni 10 kama mchango wake kusaidia kampeni za Wagombea wa Urais wa chama hicho.
Hali hiyo ilizua manung’uniko kutoka kwa baadhi ya wafuatiliaji wa mambo ya mpira nchini Tanzania, hali iliyowalazimu Young Africans kulitoa suala hilo ufafanuzi.
Katika barua yake ya Agosti 14, 2025, ilisisitiza kuwa mchango wa milioni 100 ulitolewa na taasisi ya GSM Foundation iliyo chini ya Mohamed na sio kupitia hela za wanachama au kutoka kwenye mfuko wa klabu, kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato.
Kupitia harambee hiyo, CCM ilikusanya jumla ya shilingi bilioni 86, huku kiasi cha bilioni 56.3 zikiwa zimelipwa papohapo, huku zaidi ya shilingi bilioni 30.2, zikiwa ni ahadi bilioni ni ahadi zinazotarajiwa kulipwa.