Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza kuwa maafisa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda wamekutana Washington, DC siku ya Jumatano kwa mkutano wa pili wa ufuatiliaji wa makubaliano ya amani ya Juni 27.
Katika taarifa, wajumbe wa kamati walikiri kuwepo kwa ucheleweshwaji wa kutekeleza lakini wakaeleza dhamira yao ya kuendeleza amani na usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Makubaliano hayo, yaliyotiwa saini Washington, yanatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kati ya majeshi ya nchi hizo majirani.
Mashariki mwa DRC imekumbwa na mapigano kwa miongo kadhaa. Kurejea tena kwa kundi la waasi la M23 mwaka 2021 kumetatiza zaidi hali.
Mapigano mabaya
Mapigano kati ya M23 na vikosi vya serikali mashariki mwa DRC yamesababisha watu wasiopungua 500,000 kuondolewa kwenye makazi yao na mauaji ya watu zaidi ya 3,000 kufikia mwishoni mwa mwezi Februari, kulingana na Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati cha Afrika.
DRC na Rwanda wameeleza dhamira zao katika hatua za kiufundi, kijasusi, na njia za kijeshi wakijiandaa kwa mkutano wa Doha, taarifa hiyo ilisema.
Kamati hiyo ilijumuisha wawakilishi kutoka Marekani, Qatar, Togo (kama waratibu wa Muungano wa Afrika) na Tume ya Muungano wa Afrika.