Ni mechi ya kundi B itachezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa mbili usiku za Afrika Mashariki.
Baada ya mechi yao ya ufunguzi ambapo ilikuwa timu ya kwanza kupata ushindi katika CHAN 2024, Taifa Stars inaongoza kundi hilo ikiwa na alama tatu.
Mauritania na Madagascar wote wana alama moja kila mmoja baada ya kutoka sare ya sifuri kwa sifuri katika mechi yao ya kwanza.
Kundi hilo lina timu tano na Jamhuri ya Afrika ya Kati nayo ndiyo inacheza mechi yake ya kwanza leo ikiwa dhidi ya Burkina Faso.
Vijana wa Taifa Stars wa Hemed Suleiman ‘Morocco’ wanafahamu kibarua kinachowasubiri.
Akizungumza na waandishi wa habari, kocha ‘Morocco’ anasema kikosi chake kiko tayari kuwakabili Lions of Chinguetti au Al-Murabitun ambao nao wanatafuta ushindi wao wa kwanza.
Kocha wa Mauritania Artiz Lopez Garai nae ana matumaini kuwa timu yake iko tayari kukabiliana na vijana wa Bongo.
Iwapo Tanzania watapata ushindi kwenye mechi hii ya pili, watakuwa wamejiweka katika nafasi nzuri ya kuingia katika hatua ya muondoano.
Kwenye kundi hili B ambapo mechi zake zote zinachezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam pia kuna Madagascar miongoni mwa timu hizo tano.
Katika mechi ya kwanza, kiungo mchezeshaji wa Tanzania Faisal Salum ‘Fei Toto’ alikuwa mchezaji bora wa mchuano huo.
Je, leo Taifa Stars itang’ara tena kwa Mkapa?