Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki Fahrettin Altun amesisitiza Ankara itaendelea kuunga mkono amani na mshikamano na watu wa Syria, akisisitiza kwamba uhusiano kati ya mataifa hayo mawili unaenda zaidi ya ujirani wa kijiografia, msingi wake katika uhusiano wa kitamaduni, kihistoria na kidini.
Katika ujumbe kwa jopo lenye mada "Ushirikiano kuelekea Njia ya Amani na Utulivu: Udugu wa Uturuki-Syria" uliofanyika Damascus siku ya Jumanne, Altun alisema kuwa uhusiano wa kindugu ulidumu hata wakati wa utawala mkali wa chama cha Baath, ambao alisema ulisababisha "mateso yasiyopimika" kwa watu wa Syria.
"Utawala wa Baath, ambao ulisababisha vifo vya mamia kwa maelfu na mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu katika historia ya hivi karibuni, tunashukuru umefikia kikomo," Altun alisema.
"Ninaamini watu wa Syria sasa wanaelekea kwenye mustakabali mzuri zaidi, wenye amani na matumaini."
Alisisitiza msimamo thabiti wa Uturuki katika kusimama na wanaodhulumiwa katika historia yote, na haswa wakati wa miaka ya machungu zaidi ya Syria, akipongeza uungaji mkono usioyumba wa Rais Recep Tayyip Erdogan kwa Wasyria.
Altun aliangazia usaidizi wa kina wa Uturuki wakati wa mzozo, kutoka kwa misaada ya kibinadamu hadi huduma za afya, elimu na msaada kwa Wasyria waliokimbia makazi yao, ndani ya Uturuki na kwenye mpaka.
Taasisi kama vile AFAD, Hilali Nyekundu ya Uturuki na TIKA zilichukua nafasi muhimu, alibainisha.
Kukua kwa ushirikiano katika nyanja mbalimbali
Akithibitisha kuunga mkono Uturuki kwa nchi ya Syria ambayo iko huru kuamua mustakabali wake, Altun alisema juhudi zinaendelea kuimarisha ushirikiano katika nyanja zote.
"Baada ya kufunguliwa tena kwa ubalozi wetu huko Damascus, ubalozi wetu mdogo huko Aleppo sasa unafanya kazi. Shirika la ndege la Uturuki limeanza tena safari za kuelekea mji mkuu wa Syria," alisema, akiongeza kuwa ziara za nchi mbili na ushirikiano katika usafiri wa anga, biashara, afya na nishati zimeanza kushika kasi.
Altun pia alisisitiza umuhimu wa juhudi za pamoja katika vyombo vya habari, mawasiliano, diplomasia ya umma na kupambana na taarifa potofu, akibainisha uratibu wa karibu na Wizara ya Habari ya Syria.
Ameelezea imani kuwa jopo hilo litasaidia kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Hafla hiyo ilileta pamoja wasomi, waandishi wa habari, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), maafisa na washiriki wa kimataifa.
Majadiliano yalilenga mustakabali wa ushirikiano baina ya nchi mbili katika maeneo muhimu kama vile vyombo vya habari, mawasiliano na kujenga upya mshikamano wa kijamii nchini Syria.
Jopo lilihitimisha kwa kuonyeshwa filamu ya hali halisi iliyoitwa "Mgogoro wa Syria: Diplomasia ya Amani ya Uturuki” iliyoandaliwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.