UTURUKI
2 dk kusoma
Mke wa Rais wa Uturuki ataka elimu ya kimataifa inayozingatia maadili katika mkutano wa Kiev
Emine Erdogan amesisitiza elimu kuwa nyenzo muhimu ya kukabiliana na migogoro ya dunia, akieleza juhudi za Uturuki zinazolenga utu.
Mke wa Rais wa Uturuki ataka elimu ya kimataifa inayozingatia maadili katika mkutano wa Kiev
Mke wa Rais wa Uturuki ameangazia mchango wa Uturuki katika kuimarisha elimu inayozingatia utu . / Picha: / Reuters
tokea masaa 11

Mke wa Rais wa Uturuki, Emine Erdogan, ameshiriki katika Mkutano wa Tano wa Wake na Waume wa Rais, ulioandaliwa na Mke wa Rais wa Ukraine, Olena Zelenska, jijini Kiev, ambapo alilihutubia kongamano hilo kwa njia ya video.

Mkutano huo, uliofanyika chini ya kaulimbiu "Elimu Inayobadilisha Ulimwengu," uliwakutanisha wake na waume wa marais, wataalamu wa kimataifa na watunga sera kujadili jinsi elimu inavyoweza kujenga ustahimilivu, amani, na maendeleo ya kijamii.

Pia, uliwasilisha matokeo ya utafiti wa kimataifa uliofanyika katika nchi 14 (ikiwemo Uturuki), kuhusu: "Elimu kama Chombo cha Kujenga Ustahimilivu Binafsi, Mtaji wa Kijamii wa Kitaifa, na Utamaduni wa Amani." Utafiti huo ulihusisha maoni ya wanafunzi, walimu na wazazi.

Katika hotuba yake, Emine Erdogan alielezea elimu kuwa silaha yenye nguvu zaidi ya kukabiliana na migogoro ya sasa duniani.

“Katika dunia inayopitia masaibu ya njaa, umasikini, vita, uhamiaji na mabadiliko ya tabianchi, nguvu pekee inayoweza kuinua tena ubinadamu ni elimu,” alisema, akiongeza kuwa ni kupitia mifumo ya elimu inayojikita kwenye maadili na utu, pamoja na upatikanaji wa elimu kwa wote, ndipo dunia yenye haki na usawa inaweza kujengwa.

Pia alielezea juhudi za Uturuki katika kuendeleza elimu yenye misingi ya kibinadamu, akilitaja Shirika la Maarif la Uturuki (Türkiye Maarif Foundation), linalofanya kazi katika nchi 55, kama taasisi inayoongoza katika kutoa elimu jumuishi na yenye mwelekeo wa amani.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa watoto walioko katika mazingira magumu wanatimiza haki yao ya kupata elimu, na waweze kushiriki kikamilifu katika dunia ya baadaye kwa usawa,” alisisitiza.

Alimaliza kwa kutoa shukrani kwa waandaaji wa mkutano huo na kueleza matumaini yake ya kuwa na “mustakbali uliojaa matumaini, ambapo migogoro ya kibinadamu itabaki tu kuwa historia.”

“Natumai mkutano huu muhimu, unaochangia mustakabali wa pamoja wa ubinadamu, utakuwa mwanzo wa enzi mpya.”

CHANZO:TRT World and Agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us