Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wanamgambo wa M23 wameanza tena mazungumzo ya amani huko Doha, mpatanishi wa kutoka Qatar alisema Jumanne, kufuatia ripoti za ghasia katika eneo la mashariki mwa DRC.
"Tumezipokea pande zote mbili hapa Doha kutoka DRC na M23" kujadili utekelezaji wa makubaliano ya awali, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed al-Ansari aliambia mkutano wa habari.
Serikali ya Congo na M23 walitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano mjini Doha mwezi Julai yenye lengo la kukomesha kabisa mapigano ambayo yameharibu eneo la mashariki mwa DRC lenye utajiri wa madini.
Chini ya masharti ya makubaliano hayo, pande hizo mbili zilipaswa kuanza mazungumzo ya amani Agosti 8 na kukamilisha makubaliano ifikapo Agosti 18, hata hivyo makataa yote mawili yameisha.
'Kubadilishana kwa wafungwa'
Ansari alisema mazungumzo ya sasa "yalijumuisha majadiliano ya kutafuta utaratibu wa kufuatilia usitishaji mapigano, pamoja na kubadilishana wafungwa".
"Pande zote mbili bado ziko Doha kujadili masuala haya," alisema, akiongeza mazungumzo yaliratibiwa na Marekani na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu.
Makubaliano hayo ya Julai yalifuatia makubaliano ya awali, tofauti ya amani kati ya serikali ya Congo na Rwanda yaliyotiwa saini mjini Washington.
Kundi la M23 lilikuwa limesisitiza kutafuta makubaliano yake ya kusitisha mapigano na Kinshasa, likisema kwamba mkataba wa DRC-Rwanda uliotiwa saini mwezi Juni uliacha masuala ambayo bado yanahitaji kushughulikiwa.
Makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano mashariki mwa DRC yamesambaratika, na mapema mwezi huu ripoti zilisema mapigano yalizuka kati ya jeshi la Congo na M23 licha ya kuwa na makubaliano ya usitishaji vita.