AFRIKA
2 dk kusoma
DRC, waasi wa M23 wako Qatar kwa mazungumzo ya makubaliano zaidi: mwanadiplomasia
Wajumbe kutoka DRC na kundi la waasi la M23 wamewasili nchini Qatar kwa mazungumzo ya makubaliano mapana, mwanadiplomasia anayefahamu kuhusu mazungumzo hayo ameliambia shirika la AFP.
DRC, waasi wa M23 wako Qatar kwa mazungumzo ya makubaliano zaidi: mwanadiplomasia
Waasi wa M23 walidhibiti maeneo makubwa ya mashariki mwa DRC mapema 2025. / Picha: Reuters
9 Julai 2025

Wajumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kundi la waasi la M23 walikuwa nchini Qatar Jumatano kwa mazungumzo mapana kuhusu makubaliano, mwanadiplomasia anayefahamu yanayojiri kuhusu mazungumzo hayo ameliambia shirika la AFP.

"Wajumbe kutoka pande zote za DRC na ... M23 wako mjini Doha, huku Qatar wakiwa wapatanishi wa mazungumzo hayo," mwanadiplomasia ameliambia shirika la habari la AFP, akizungumza kwa masharti ya kutotambuliwa kwa sababu ya namna majadiliano yalivyo nyeti.

Kundi la M23, ambalo linasemekana kuungwa mkono na Rwanda, wiki iliopita lilitaka mazungumzo zaidi kuzungumzia matatizo ambayo hayakujumuishwa kwenye makubaliano ya amani yaliyotiwa saini kati ya Rwanda na DRC jijini Washington mwezi Juni.

"Hatua hii ya majadiliano itakuwa muhimu sana katika kufikia makubaliano," mwanadiplomasia alisema, akiongeza kuwa wapatanishi wa Qatar walikuwa wanafanya kazi pamoja na Umoja wa Afrika.

Mapigano makali

Makubaliano hayo ya DRC na Rwanda yalikuwa yanalenga kumaliza mapigano ambayo yamesababisha vifo ya maelfu katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa DRC.

Lakini M23, kundi kubwa linalopigana na wanajeshi wa Congo, hawakuwepo kwenye mazungumzo ya Washington na kutaka kuwepo kwa makubaliano mengine ya kusitisha mapigano na serikali ya DRC.

M23 ilichukuwa udhibiti wa maeneo ya mashariki mwa DRC kupitia mapigano makali mwezi Januari na Februari, ikiwemo miji mikuu ya mikoa ya Goma na Bukavu.

Mapigano yametatiza mashariki mwa DRC kwa miongo zaidi ya mitatu, na kusababisha maelfu ya watu kuhama katika makazi yao.

Rwanda inakanusha kuunga mkono M23

Rwanda inakanusha kuwapa msaada wa kijeshi kundi hilo, lakini wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema jeshi la Rwanda limekuwa na jukumu "la msingi" katika makabiliano ya M23, ikiwemo mapigano ya kijeshi.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us