Timu ya Taifa ya soka ya Uganda, Uganda Cranes imekosa kitita cha zaidi ya dola 330,000 ambacho Rais Yoweri Museveni aliahidi atawapa wakishinda kila mechi katika michuano ya wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani, CHAN 2024.
Katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Algeria 4 Agosti, kwenye uwanja wa taifa wa Mandela Namboole, walizabwa magoli 3 kwa sifuri.
Wenzao nchini Kenya, Harambee Stars wana tabasamu kubwa ikiwa tayari zaidi ya dola 7,000 ziko katika akaunti zao.
Rais William Ruto aliwaahidi shilingi milioni moja ya Keya kwa kila mechi watakayoshinda na walipoicharaza DRC katika mechi yao ya kwanza 3 Agosti 2025, Ruto alitimiza ahadi yake.
Taifa Stars ya Tanzania pia tayari wamepokea zaidi ya dola 7,900 kama timu (shilingi milioni 20) kutoka kwa ahadi ya Rais Samia Suluhu baada ya kushinda mechi yao ya kwanza ambayo ilikuwa ya ufunguzi wa michuano dhidi ya Burkina Faso tarehe 2 Agosti.
Hebu sasa tuangalie utajiri wa wachezaji hawa iwapo watashinda michuano ya CHAN 2024.
Timu ya Uganda Cranes sasa ina matumaini kwa mechi tatu zilizobaki kwenye hatua za makundi, wakishinda basi watapata zaidi ya dola 990,000 ikiwa ni ahadi ya rais Yoweri Museveni.
Taifa Stars ya Tanzania nayo ikifanikiwa kushinda mechi zake zilizobaki za CHAN watawapa zaidi ya dola 3900 kwa kila goli na nyongeza ya zaidi ya dola 390,000 au shilingi bilioni 1 za Tanzania iwapo watatwaa ubingwa, ikiwa ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kila mchezaji na benchi la ufundi la Harambee Stars ya Kenya atapata zaidi ya dola 28,000 iwapo watashinda mechi zote za hatua ya makundi.
Kwa kila matokeo ya sare kila mchezaji atachukua takriban dola 3,800 (shilingi 500,000).
Na iwapo Harambee Stars itanyanyua kombe la CHAN timu itapata takriban dola milioni 4.6 ikiwa ni shilingi milioni 600 za Kenya kutoka kwa Rais.
Rais pia ameahidi “kuwapanga” katika mradi wa nyumba ambazo serikali inajenga za bei nafuu.
Tumeangazia tu nchi tatu katika michuano hii ya CHAN 2024.
Kuna zingine 16 ambazo huenda marais au viongozi wao wa nchi wametangaza au watatangaza zawadi mbalimbali kwa timu zao wakati wa michuano au hata mwisho wake kama njia ya kuwahamasisha.
Zawadi kutoka CAF
Shirikisho la soka barani Afrika CAF nalo limetenga zawadi kwa washindi.
Timu itakayotwaa ubingwa itapata dola milioni 3.5.
Mshindi wa pili atabeba kitita cha dola milioni 1.2
Wa tatu atakwenda nyumbani na dola 700,000, huku wa nne akitia kibindoni dola laki sita.
Kwa hivyo sasa kazi ni kwa kila timu kuona namna gani watajituma wapata fedha za CAF pamoja na zile walizoahidiwa na marais.
Yote tisa, kumi maamuzi yote yatafanyika uwanjani na hapo tutafahamu nani ataweka kitita cha kutosha kibindoni.