Uganda imeingia makubaliano na Marekani kupokea raia kutoka nchi za tatu ambao huenda wasipate hifadhi nchini Marekani lakini hawako tayari kurejea katika nchi zao za asili, Wizara ya Mambo ya Nje imesema Alhamisi.
"Huu ni mpango wa muda mfupi wenye masharti, ikiwa ni pamoja na kwamba watu wenye rekodi za uhalifu na watoto wasiokuwa na walezi hawatakubaliwa," alisema Vincent Bagiire Waiswa, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, katika taarifa yake.
Uganda inakuwa nchi ya hivi karibuni barani Afrika kukubali wahamiaji waliorejeshwa kutoka Marekani baada ya Eswatini, Sudan Kusini, na Rwanda kufikia makubaliano kama hayo na Marekani.
Rais Donald Trump analenga kuwafukuza mamilioni ya wahamiaji walioko nchini Marekani kinyume cha sheria, na serikali yake imekuwa ikijitahidi kuongeza idadi ya wahamiaji wanaorejeshwa katika nchi za tatu.
Wapinzani wamekosoa hatua hizi za kuwafukuza wahamiaji wakisema ni hatari na za kikatili, kwani watu wanaweza kutumwa katika nchi ambazo hawana uhusiano nazo na hawazungumzi lugha ya wenyeji.
Mahakama Kuu ya Marekani mnamo Juni iliruhusu serikali ya Trump kuwafukuza wahamiaji kwenda nchi za tatu bila kuwapa nafasi ya kuonyesha kuwa wanaweza kuathirika.
Hata hivyo, awali, nchi hiyo ilikana taarifa za kuwepo kwa mpango huo.