Lango la Afrika kuelekea Mwezini: Somalia yajiandaa kufika anga za mbali kwa msaada wa Uturuki
AFRIKA
4 dk kusoma
Lango la Afrika kuelekea Mwezini: Somalia yajiandaa kufika anga za mbali kwa msaada wa UturukiUturuki inaisaidia Somalia kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuzindua satelaiti kutoka katika ardhi yenyewe, kwa kutumia uwekezaji wa dola bilioni 6.
Bunge la Somalia limeidhinisha mradi huo, ikionyesha uungwaji mkono mpana wa kisiasa. / / Wengine
tokea siku moja

Somalia inajiandaa kuwa nchi ya kwanza Afrika kuanzisha uzinduzi wa satelaiti kutoka ardhini mwake, hatua ambayo wengi wasingeweza kuiona, hasa kwa taifa ambalo linalojijenga upya baada ya miaka zaidi ya 30 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ushirikiano wa anga wa dola bilioni 6 za Marekani kati ya Somalia na Uturuki unakuja miaka 13 tu baada ya Somalia kuunda serikali ya shirikisho, wakati msaada wa kimataifa ulikuwa ukielekezwa hasa kwenye usalama na miundombinu.

Hivi sasa, kituo cha anga za mbali kinaendelea kujengwa kando ya pwani ya Bahari ya Hindi, huku uzinduzi wa kwanza ukitarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2025.

"Kuanzisha satelaiti kutoka Somalia kwenda angani ni mafanikio makubwa, zaidi ya thamani ya mabilioni ya dola," amesema Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, kuhusu mpango huo.

Ushirikiano na Uturuki ni mojawapo ya uwekezaji mkubwa wa kigeni katika historia ya Somalia na unaashiria mabadiliko makubwa katika vipaumbele vya kimkakati vya mataifa haya mawili, hasa kwa kutumia fursa ya maendeleo ya kiuchumi na kisayansi.

Manufaa kijiografia

Somalia ipo juu ya mstari wa ikweta, ikivuka hemisfia ya Kaskazini na Kusini na hivyo kuifanya kuwa miongoni mwa maeneo bora zaidi duniani kwa uzinduzi wa roketi.

Roketi zinazozinduliwa kutoka maeneo ya ikweta hupata mwendo wa juu zaidi wa mzunguko wa dunia – karibu kilomita 1,670 kwa saa – na hivyo kupunguza matumizi ya mafuta na kuongeza uwezo wa kubeba mizigo.

Eneo la kilomita 30 kwa 30 lililochaguliwa kando ya pwani ya Somalia, yenye urefu zaidi barani Afrika, pia lina njia za wazi kuelekea mashariki juu ya Bahari ya Hindi, hivyo kuhakikisha vipande vya roketi vinavyorudi duniani, havianguki karibu na maeneo ya makazi.

Ushirikiano unaofaidisha pande zote

Kituo hiki cha anga kinakidhi malengo muhimu ya ramani ya miongo 10 ya sekta ya anga ya Uturuki iliyotangazwa mwaka 2021, ikiwemo mipango ya kufikia kutua kwa roketi mwezini ifikapo 2028, kujenga Mfumo wa Kitaifa wa Uelekezaji wa Satelaiti unaolingana na GPS, na kupima uwezo wa makombora ya umbali mrefu.

Eneo hili linaipa Uturuki jukwaa la uzinduzi mbali na NATO, likitoa fursa za kisiasa na uwezo wa kupima uzito wa zana za kijeshi pamoja na satelaiti za kiraia.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, aliripotiwa kutoa "habari njema" kuhusu maandalizi ya ujenzi wa kituo hiki cha anga katika mkutano wa ndani na kamati kuu ya chama tawala cha AK.

Maafisa wa ulinzi wa Uturuki wamebainisha kuwa kituo hicho kitakuwa pia ni kituo cha majaribio ya makombora ya masafa mrefu, kinachounga mkono mifumo ya makombora ya Tayfun na Cenk, yal iliyoundwa kwa mashambulio ya masafa marefu, na hivyo kutumika kwa shughuli mbili, za anga na ulinzi.

Kwa upande wa Somalia, uwanja huu wa anga unaahidi faida za kiuchumi zisizowahi kuonekana, zikiwemo ajira katika ujenzi, usafirishaji na sekta za sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabati.

Masharti ya uhamisho wa teknolojia na programu za mafunzo yaliyowekwa katika makubaliano yanalenga kukuza wataalamu wa ndani katika nyanja za anga na viwanda vinavyohusiana na mradi huo.

"Ninaamini kuwa faida za kimkakati za muda mrefu za mradi huu ni kubwa zaidi kuliko faida za kifedha za papo kwa hapo. Mradi huu utakuwa kichocheo cha maarifa na ubunifu, utazalisha ujuzi mpya, kujenga uwezo kwa vijana wetu, na kuunda ajira mpya," asema Rais Mohamud.

"Sehemu muhimu ya makubaliano ni kuimarisha msingi wa maarifa kwa vijana wa Somalia, hivyo kuwezesha kuibuka kwa viwanda na huduma mpya."

Bunge la Somalia tayari limeidhinisha mradi huo, kuashiria msaada mpana wa kisiasa licha ya uwekezaji mkubwa wa mabilioni ya dola.

Athari za kanda

Uwekezaji wa Uturuki Somalia ni sehemu ya mkakati wake wa kushirikiana zaidi na Afrika na kuimarisha ushirikiano “unaofaidisha pande zote” katika bara hilo.

Uwepo wa Uturuki Pembe ya Afrika umekuwa ukihusisha mafunzo ya kijeshi, uendeshaji wa bandari na utoaji wa misaada ya kibinadamu. Uwanja wa anga Somalia ni hatua kubwa zaidi ya malengo.

Badala ya msaada wa maendeleo wa kawaida, mradi huu unaiweka Uturuki kama mdau muhimu wa kimataifa katika teknolojia za juu katika eneo la anga za mbali.

Mataifa haya mawili yanajiwekea dau kubwa kwenye ushirikiano unaoonekana wa kipekee. Somalia inapata teknolojia ya kisasa na ajira za kutosha huku Uturuki ikipata eneo la uzinduzi karibu na mstari wa ikweta lenye kukidhi mahitaji yake.

Muda wa kuelekea katika enzi mpya ya ushirikiano umeanza.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us