Na Ronald Sonyo, TRT Afrika Dodoma
Changamoto hizi zinatokana na sababu kadhaa ikiwemo, uhaba wa viwanda vya uchenjuaji na kuyeyusha madini ili kuongezea thamani.
Hata hivyo, Serikali ya nchi hiyo imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ya kukabiliana na changamoto hizo, kwa kujenga viwanda vipya na kuweka sheria kali inayokusudia kulinda wazalishaji wa ndani.
Hatua hizi zinakusudia kuhakikisha wachimbaji wananufaika moja kwa moja na rasilimali hizo.
Kwa sasa, miradi kadhaa ya viwanda vya kuongeza thamani ya madini ipo katika hatua za utekelezaji, ikiwemo kiwanda kitakachochakata zaidi ya tani 200,000 za nikeli na shaba kwa mwaka.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha kusafisha na kusindika madini hayo kinachojengwa na Kampuni ya Zhongzhou Mining Co. Ltd, eneo la Zamahero, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema Tanzania inalenga kuwa kitovu cha uchumi wa kijani, hasa katika kutengeneza magari ya umeme, betri za magari, nishati safi na vifaa vya kielektroniki.
/
“Ujenzi wa kiwanda hiki ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kuongeza thamani ya madini nchini. Tunataka kuona Tanzania ikibadilika na kuwa taifa linalozalisha bidhaa zenye thamani kubwa kwenye soko la dunia la teknolojia,” amesema Mavunde.
Waziri huyo ameeleza kuwa mradi huo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 15 utakapokamilika utazalisha takribani tani 200,000 za nikeli na shaba kwa mwaka, na kutoa ajira kwa mamia ya watanzania.
“Uwekezaji huu ni kielelezo cha mafanikio ya Serikali katika kufanikisha dira ya uchumi wa viwanda na uongezaji thamani madini” ameongeza
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga amesema kuwa, uwekezaji kwenye miradi ya kuongeza thamani, Tanzania inajenga msingi imara wa ajira, mapato, na uchumi shindani kimataifa.
Aidha, Serikali imetenga Shilingi bilioni 14.3 za Kitanzania kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya kisasa ya sampuli za madini (GST), itakayokuwa ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, maabara hiyo itakuwa ya pili baada ya ile ya Mintek nchini Afrika Kusini.
Sekta ya madini inatajwa kuwa miongoni mwa sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Hata hivyo, wananchi wengi bado wanasubiri kuona ni kwa kiwango gani miradi hii mipya itabadilisha maisha ya wachimbaji wadogo, ambao kwa asilimia kubwa hutegemea shughuli za uchimbaji kama kipato chao kikuu.