Rais Recep Tayyip Erdogan amethibitisha tena uungaji mkono wa Uturuki kwa watu wa Palestina, huku akitoa ukosoaji mkali dhidi ya uongozi wa Israel.
"Katika siku hizi ngumu ambapo serikali ya Netanyahu imepoteza kabisa mwelekeo, tunasimama na watu waliodhulumiwa wa Gaza kwa kutumia kila njia tuliyonayo," alisema Erdogan siku ya Jumatatu kupitia hotuba ya televisheni kwa taifa baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri.
“Licha ya shinikizo zote, vitisho, kiburi na hali ya kutokuwajibika ya mtandao wa wauaji walioua zaidi ya watu wasio na hatia 64,000, bado tunashikilia msimamo wetu thabiti,” alisema Erdogan.
“Inshallah, tutaendeleza msimamo huo huo wa dhamira katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ujao na kuwa sauti ya Wapalestina waliodhulumiwa huko.”
Uvamizi wa kijeshi wa Israel dhidi ya Gaza, ambao wengi wanaoushuhudia wanautaja kuwa ni mauaji ya halaiki, umeingia siku ya 702, huku Wapalestina 64,522 wakiwa wameuawa, wakiwemo 393 waliokufa kwa njaa iliyosababishwa kimaksudi na Israel.
Malengo ya nishati ya nyuklia kupitia mradi wa Akkuyu
Rais pia alizungumzia malengo ya Uturuki katika sekta ya nishati, akielezea maendeleo ya mradi wa Kinu cha Nyuklia cha Akkuyu.
Kwa uwezo wa jumla wa uzalishaji wa megawati 4,800, Erdogan alisema kinu hicho kitasadia Uturuki "kubadili bahati yake" na kuimarisha kujitegemea kwake katika sekta ya nishati.
Nishati ya nyuklia ina nafasi muhimu katika kufanikisha lengo la Uturuki bila hewa chafu ifikapo mwaka 2053. Kwa mantiki hiyo, nchi hiyo inapanga kujenga viwanda vingine vya nyuklia katika maeneo mawili zaidi baada ya kinu cha kwanza cha Akkuyu.
Mkataba wa ushirikiano wa kiserikali ulisainiwa kati ya Russia na Uturuki mnamo Mei 2010 kwa ajili ya ujenzi wa Kinu cha Nyuklia cha Akkuyu (Akkuyu NPP), ambacho kitakuwa na mitambo minne ya nguvu aina ya VVER-1200, zenye jumla ya uwezo wa megawati 4,800.
Msingi wa mradi huo uliwekwa mwaka 2018, na kulingana na mkataba, unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka saba.