Algeria iliichabanga Uganda jumla ya mabao matatu kwa nunge, katika mechi ya kwanza ya Kundi C ya michuano ya CHAN 2024, uliofanyika katika uwanja wa taifa wa Mandela wa jijini Kampala, siku ya Agosti 4.
Matokeo hayo, yanaifanya Uganda kuwa mwenyeji wa kwanza kupoteza mchezo wao wa ufunguzi, kufuatia ushindi wa Tanzania na Kenya.
Bao la kwanza la Algeria, lilitiwa kimiani na Ayoub Ghezala, akiruka juu na kukutana na krosi ya Abderrahmane Meziane katika dakika ya 36 ya mchezo.
Meziane, ambaye alitangazwa kama mchezaji bora wa mechi hiyo, alitia nyavuni bao lake katika dakika ya 76, kabla ya Sofiane Bayazid kugongelea msumari kwenye jeneza la ‘The Cranes’, dakika tatu baadaye.
Bao hilo, liliamsha hasira ya mashabiki wa Uganda, ambao walilazimika kutoka nje ya uwanja wa Mandela, wakimuacha nyuma mke wa rais Yoweri Museveni, Janet Museveni uwanjani.