Fundi cherehani asiyeona na simulizi ya njiti ya ufagio
Fundi cherehani asiyeona na simulizi ya njiti ya ufagio
Fundi cherehani huyo alipoteza uwezo wa kuona mwaka 2014 baada ya kuugua ugonjwa wa trakoma, ambao hutanua mboni za macho.
20 Agosti 2025

Ukipita karibu na ofisi yake ya kushonea, huenda usigundue kuwa mwendeshaji wa ofisi hiyo ana changamoto ya kuona.

“Nimefanya kazi hii kwa miaka 34 sasa, na ndiyo kazi pekee ninayoijua kwa kweli,” anasema Charles Kibe Mwangi, fundi cherehani mwenye changamoto ya kuona, katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Huku ulimwengu ukigeuka giza mbele ya macho yake, Charles aligeukia fimbo yake ya ufagio, kama rafiki yake na tegemeo lake pekee anapojaribu kutembea kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Hata hivyo, hakuruhusu ulemavu wake kuwa kizuizi kwake katika shughuli za kumpatia riziki yake ya kila siku, yaani ushonaji.

Kulingana na Mwangi, ilikuwa ni njiti ya ufagio iliyomsukuma kuendelea na shughuli ya ushonaji licha ya kupoteza uwezo wa kuona.

Ni kijiti hicho hicho, kilichomuzewesha kutunga uzi kwenye mashine ya kushonea ngumu, kitu ambacho hakuweza kufanya hapo awali.

“Kijiti hichi kimebasilisha kabisa maisha yanu,” anasema Mwangi kwa upole, huku akitoa kijiti hicho nyuma ya sikio lake la kushoto, ambako ndiko anapokihifadhi.

Kila anaposhika njiti hiyo kila siku na kuhisi wembamba wake kwenye vidole vyake, Mwangi hupata ujasiri na kuamini kwamba ana suluhisho la kudumu la kuanzisha kazi yake kila asubuhi.

Ili aweze kuifahamu vyema futi yake ya kupimia nguo, Mwangi alimuomba rafiki yake mmoja ili aweze kumuwekea alama kuanzia sentimita moja hadi sitini kwa kutumia nukta nundu(Braille).

“Kazi ya kushona inahitaji vipimo kamili na halisia,” anaeleza kwa kujiamini na tabasamu kubwa usoni mwake.

“Kama mtu anasema suruali yake ni inchi 12, inapaswa kuwa inchi 12. Nimebobea kwenye hili kwa miaka mingi sasa na nguo zote ninazozishona huwa na vipimo sahihi, kulingana na mahitaji ya mteja.”

Wateja wake humsaidia kwa kumtambua rangi za vitambaa na nyuzi.

 “Nimemfahamu Kibe kwa muda mrefu tangu watoto wangu walipokuwa wadogo, mtoto wangu mdogo sasa ana umri wa miaka 32. Aliwashonea nguo watoto wangu na sasa anawatengenezea wajukuu zangu,” anaeleza Margaret Gathecha, mteja wake wa muda mrefu.

Kibe anakiri kuwa alipoteza baadhi ya wateja baada ya kupata ulemavu wa macho, lakini mbinu mpya alizozitumia zimeendelea kumuwezesha kuendesha biashara huku akihakikisha wateja wake wanaridhika na kila mshono unaopitia mikononi mwake.

Kama anavyosema mwenyewe, alipoteza uwezo wa kuona mwaka 2014 baada ya kuugua ugonjwa wa trakoma, ambao hutanua mboni za jicho.

 Alipofuka kabisa ilipofika mwaka 2017.

Mwangi ana matumaini kuwa siku moja Mungu atarudisha uoni wake, ili aweze kuangalia uso wa watoto wake waliokomaa na kuona mabadiliko yao kwa kweli baada ya miaka mingi.

“Natamani kuwaona watoto wangu, japo  sina kumbukumbu za nyuso zao, kama Mungu atataka nione tena, hiyo ndio ndoto yangu kubwa. Nataka sana kuona nyuso zao.”

Japo anakumbana na changamoto nyingi, anakataa kufikiria maisha ya baadaye ambapo atatembea mitaani akibeba bakuli la kuomba msaada kutoka kwa wapita njia.

“Sijawahi kufikiria kuwa nitakuwa nikiomba mitaani,” anasema.

“Ninaamini katika ufundi wangu, ndio unaonilea mimi na familia yangu. Nitaendelea kufanya kazi, na kama mtu yeyote atahisi kusaidia, wanaweza kufanya hivyo kupitia kazi ninazozifanya hapa.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us