Kampuni ya kifahari Prada na mzozo wa 'Kubazi'
Kampuni ya kifahari Prada na mzozo wa 'Kubazi'
Prada imejikuta katika vita vikubwa vya mtandaoni baada ya kuzindua toleo lake la 2026 la mtindo wa viatu vya kiume, unaoaminiwa kuigwa kutoka kwa Wahindi.
5 Agosti 2025

Prada ilipozindua wanamitindo wake katika maonyesho ya kifahari ya Wiki ya Fasheni ya Milan mwezi Julai, haikutarajia mapokezi iliyopata.

Mojawapo ya uzinduzi wake ilikuwa ni viatu aina ya makubadhi (kubazi), ambavyo vinafanana sana na champali za kihindi kutoka eneo la Maharashtra. Na hapo ndivyo vita vya mtandaoni vilipozuka.

Wahindi waliochagia vita hivyo walidai kuwa ubunifu wa viatu hivyo ni wizi wa mtindo wa viatu vya asili vilivyovaliwa na jamii hiyo kwa zaidi ya miaka mia moja.

Prada, kampuni ya mavazi ya kifahari ya Kitaliano inayouza makubadhi haya kwa takriban dola 1200 ambapo ukinunua nchini India unaweza kuvipata viatu hivyo kwa gharama ya chini ya dola 20.

Walalamikaji hao wameishutumu Prada madai ya kuiba utambulisho wa zaidi ya karne moja wa jamii yao jambo ambalo wanasema linatishia pato la jamii hiyo inayotegemea mauzo ya viatu hivyo.

Hatimaye Prada wameonekana kusalimu amri kutokana na shinikizo la mtandaoni na wamejibu kupitia ukurasa wa Instagram kwa kukiri kuwa uasilia wa champali hizo unatoka India, na hata kusema kuwa wapo katika mashauriano na vyombo husika vya biashara na mauzo kutoka India kuhusu namna ya kuwahusisha fundi viatu wa champali hizi kutoka India katika utengenezaji, na hata mauzo yake.

Sio Kawaida kuona kampuni kubwa ya kimataifa kukiri kosa kama hili kabla hata kushtakiwa mahakamani.

Viatu hivi vya kubazi vinavaliwa sana Afrika na katika jamii ya Waswahili ambao wanaaminiwa pia wameshawishiwa kwa kiasi kikubwa na mila na tamaduni za ‘ki Asia’ hasa Wahindi, kupitia vyakula, mavazi, na viatu.

Wizi au uigizaji huu wa vitu vya asili kutoka makampuni ya kifahari ya kimataifa umekuwa ukifanywa kwa miaka mingi hata kutoka Afrika, ambapo vitu kama shuka za Kimaasai zilionekana kuigwa, vikapu vya mkonge, vikoi vya Kiswahili, shanga , na mengineyo mengi.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us