Kwa mtu ambaye nimekuwa nikisaidia kutia kasi kwa wanariadha wanaojaribu kuvunja rekodi ya dunia — ikiwemo magwiji kama kina Daniel Komen, Haile Gebrselassie, na Kenenisa Bekele—nimeona namna masuala muhimu yanavyoangaziwa ambayo yanaweza kuleta mafanikio au yakatibua historia.
Kuvunja rekodi ni mchanganyiko wa sanaa na sayansi.
Jaribio la Faith Kipyegon kutaka kuweka rekodi ya kukimbia maili moja chini ya dakika nne ilikuwa ni ujasiri na juhudi zenye kuhamasisha, lakini kuna masuala kadhaa yalitakiwa kuzingatiwa ili kufanikisha hilo.
Hizi ni baadhi ya sababu kwa nini mwanariadha huyo mwenye historia, alishindwa kwenye jaribio lake licha ya kuungwa mkono.
Watia kasi wengi, hamna mfumo
Nimesaidia kuweka kasi katika mashindano makubwa ya mbio, na siku zote lengo ni uhakika, siyo kuwa na watu wengi.
Jijini Paris, Faith alikuwa na watia kasi kumi na tatu. Wakati hili ni jambo zuri, linaweza kuwa tatizo. Wanariadha wengi uwanjani wanaweza kuleta mtafaruku, kuziba wengine, na kufanya iwe vigumu kuwa na mfumo mzuri. Badala ya kumsaidia akimbie mbio zaidi, watia kasi wanakuwa kama pingamizi.
Njia gani nzuri? Watia kasi wanatakiwa wakiwa wengi zaidi wafike wanne tu. Ikiwa imebaki mita mbili kumaliza, watia kasi walitakiwa kuondoka uwanjani, wamuache Faith amalize peke yake kwa kishindo. Hivyo ndivyo namna ya kuandaa mbio, siyo kwa kuonesha.
Udhibiti wa mbio
Kutokana na uzoefu wangu, kasi nzuri huwa haionekani. Inafanya wanariadha wahisi kuwa wanamiliki, kujiweka sawa kwa ajili ya mbio hizo, na kuwa tayari kwa ajili ya matokeo ya juhudi zao.
Jijini Paris, Faith alionekana kukwama, kiakili na kiuwezo pia. Alihitaji kuhisi kama anaongoza mbio hizo, siyo tu kuwa sehemu ya mpango mpana.
Anahitaji kupunguza muda kwa kiasi kikubwa
Faith alihitaji kupunguza muda wa sekunde 8 kutoka kwa rekodi yake mwenyewe ya dunia ya dakika 4:07.64. Katika mbio za maili moja, ambapo rekodi zinavunjwa na sehemu ndogo ya sekunde. Makosa madogo yanaweza kusababisha matatizo makubwa.
Uimara wa uwezo
Wanasayansi wa michezo waandamizi wanaamini kuwa, takwimu zilizoko sasa, hakuna mwanariadha wa kike, ikiwemo Faith, wenye uwezo imara au uthubutu unaotakiwa pamoja na kasi ya kukimbia maili moja chini ya dakika nne.
Muda wake mzuri wa mbio za mita 800 ni dakika 1:57.68, ambao ni muda mzuri, lakini inaonesha kuwa huenda asiwe na uwezo imara wa kukimbia raundi zote nne.
Mbio za kasi za mita 800 katika muda wa dakika 1.55 zingemfanya amalize chini ya dakika 4 kama angekimbia sekunde 59 kila mzunguko.
Mkakati wa mbio
Mzunguko wa tatu wa mbio za maili moja kawaida unakuwa mgumu. Mtu anakuwa na uchovu, lakini bado utepe wa kumaliza unakuwa mbali. Mzunguko huu unaamua mbio zenyewe. Hapa ndiyo ambapo alihitaji usaidizi zaidi kumalizia mzunguko wa mwisho.
Mbinu za mazoezi
Inasemekana kuwa Faith hakubadilisha mbinu zake za mazoezi kwa ajili ya mbio hizi. Pamoja na kuwa mazoezi yake yalimfanya kuweka rekodi ya dunia, wataalamu wanasema kupita kizingiti kigumu kama hicho kunahitaji mazoezi maalum zaidi.
Sheria na teknolojia
Faith alitumia viatu na nguo maalum, lakini hata teknolojia bora zaidi haiwezi kusaidia sana katika mbio za maili moja. Pia, kwa sababu hizi zilikuwa mbio za maonesho na watia kasi wanaume, muda wake usingehesabiwa kama muda rasmi wa rekodi ya dunia. Huenda hili lilibadilisha mtazamo wa ushindani.
Mbio chache
Faith amekimbia mara moja tu mapema 2025 (Mita 1000 ambapo hakuvunja rekodi ya dunia ya mbio hizo). Kukosa kushiriki mbio, za mashindano huenda kulitatiza maandalizi yake.
Anachotakiwa kufanya Faith
Faith Kipyegon ana uwezo wa kukimbia chini ya dakika nne. Lakini njia aliyotumia si sahihi. Anahitaji mpango mzuri wa kumpa nafasi, mfumo, na udhibiti. Naamini anaweza kufanikiwa, lakini wakati mwingine, mbio ziwe za kwake, siyo kwa ajili ya maonesho.
Kama kuna kitu nimejifunza katika mambo ya kutia kasi kwa ajili ya kuvunja rekodi, historia inawekwa kwa kutambua mahitaji ya mwanariadha—uwezo na kiakili, natarajia waandaaji watasikiliza:
· Watia kasi wachache, uhakika zaidi
· Wampe nafasi Faith ya kuongoza mbio
· Waandae mbio wakizingatia mwanariadha, wala siyo maonesho
Faith bado ana fursa nyingi. Ana kipaji. Lakini wakati mwingine, tuhakikishe kuwa watia kasi wana ujuzi zaidi kama mwanariadha mwenyewe.
Kwa ufupi: Jaribio la Faith kumaliza maili moja chini ya dakika nne hakukufanikiwa kwa sababu mbio zenyewe zilijikita zaidi katika maonesho kuliko kile ambacho alihitaji zaidi. Kukiwa na mtazamo wa uhakika, naamini ataweka historia.
Mwandishi, Martin Keino ni mwanariadha wa zamani wa kulipwa ambaye alisaidia kuwekwa kwa rekodi saba akiwa kama mtia kasi kati ya 1990-2005. Sasa hivi ni Mkurugenzi Mkuu wa Keino Sports Events, na mchambuzi wa hafla za kimataifa za riadha.
Kanusho: Maoni yaliyowasilishwa na mwandishi hayaakisi maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.