Ni wazi kuwa punda ni kati ya wanyama muhimu sana katika maisha ya kila siku ya binadamu.
Wako watu wanaofuga wanyama hawa kama ajili ya matumizi yao mbalimbali, kama vile ubebaji wa mizigo, na wapo wengine huamua tu kuwafuga majumbani.
Kama ulikuwa hufahamu, wanyama hawa pia hutumika kama tiba, kupitia viungo vyao, mathalani manyoya, kwato, mifupa na hata vinyesi vyao.
Mathalani, ni jambo la kawaida sana kukutana na kina mama wa Kimaasai wakiwa na punda waliobeba mizigo migongoni mwao, katika mitaa mbalimbali ya mji wa Arusha, Kaskazini mwa Tanzania.

Hata hivyo, kaskazini mwa Tanzania, wanyama hawa wanapitia madhila makubwa.
Dosari ya usalama mpakani Namanga
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kulinda Wanyama cha Arusha (ASPA), Livingstone Masija, ukosefu wa usalama na doria ya kutosha katika mpaka wa Namanga, wenye kuunganisha nchi mbili za Kenya na Tanzania, unachochea vya kutosha biashara haramu na utoroshwaji wa wanyama hawa.
Masija anasema kuwa, wanyama hawa hupitishwa katika njia zisizo rasmi, maarufu kama ‘njia za vichochoroni’, na hivyo kuwa ngumu kwa maafisa mifugo mpakani hapo kubaini biashara hiyo haramu.
“Matumizi ya njia hizi za vichochoroni inachochea pakubwa kushamiri kwa biashara ya utoroshwaji wa mnyama punda,” anasema Masija.
Inakadiriwa kuwa, kiasi cha punda milioni 100, huchangia pakubwa katika ustawi wa kaya nyingi duniani, licha ya mchango wao kutothaminiwa.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni zilizotolewa taasisi ya AIPWA, kila mwezi, punda wapatao 150 kutoka Tanzania, huingia nchini Kenya kwa njia zisizo halali.
Punda hao hurundikwa kwenye malori, bila kupewa chakula, maji na huambulia vipigo kutoka kwa wale wanaowasafirisha wawapo kwenye malori hayo.
“Hata wakihabatika kupona na kufika mwisho wa safari yao, punda hao huishia kuchinjwa kwa ajili ya ngozi,” taasisi hiyo inasema.
‘Diplomasia iliyozorota’
Kwa upande wake, Masija anaainisha kuzorota kwa diplomasia kati ya Tanzania na Kenyam hususani katika eneo la mifugo, kama moja ya sababu zilizochochea kukua kwa utoroshwaji haramu wa punda.
“Mara kwa mara tumeshuhudia mifugo ikikamatwa, kutaifishwa na hata kupigwa minada,” anaeleza.
Mwezi Julai 2024, ngamia 300 walikamatwa kwenye hifadhi ya msitu wa Mwakijembe uliopo mpakani mwa Tanzania na Kenya, wakichungwa kwa lengo la kupata malisho.
Uchache wa rasilimali watu wa kulinda eneo la mpaka imekuwa pia ni changamoto kubwa ya kupambana na utoroshwaji wa punda, kulingana na Masija.
Pia, zipo sababu nyingine kama vile rushwa, ukosefu wa uelewa kati ya jamii za mpakani kuhusiana na biashara ya ngozi ya punda.
Inadaiwa kuwa, mara baada ya kuchinjwa, sio kwa ajili ya nyama yake tu, bali ongezeko la mahitaji ya ngozi ya mnyama huyo kwa ajili ya kutengenezea dawa barani Asia.
Ongezeko la ‘mahitaji ya dawa’
Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya 'Donkey Sanctuary', punda milioni 5.9 huchinjwa kila mwaka ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya 'ejiao,' dawa ya kitamaduni ya Kichina, inayotengenezwa kwa ngozi za wanyama hao.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni zilizotolewa taasisi ya AIPWA, kila mwezi, punda wapatao 150 kutoka Tanzania, huingia nchini Kenya kwa njia zisizo halali.
Inakadiriwa kuwa, idadi hiyo inaweza kufikia milioni 6.7 ifikapo 2027.
Viwanda vyenye kutengeneza 'Ejiao' vimeongezeka maradufu, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.
Kati ya 2013 na 2016, uzalishaji wa kila mwaka wa 'ejiao' uliongezeka kutoka tani 3,200 hadi 5,600, ambao ni sawa na ukuaji wa kila mwaka wa zaidi ya asilimia 20.
Taarifa mbalimbali, pia zimeonesha uzalishaji wa 'Ejiao' ukiongezeka kwa asilimia 160, kati ya 2016 na 2021.
"Nchi za Kiafrika na nyengine kutoka Amerika Kusini ziliathirika kwa kiasi kikubwa na biashara hii," Masija anaeleza.
Madhara ya biashara hiyo haramu
Kustawi kwa biashara hiyo kunadaiwa kuipotezea mapato Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwani hufanyika pasipo kufuata sheria na bila kuhusisha malipo ya kodi.
“Pia imechangia kuongezeka kwa magonjwa ya punda, kwani wale wagonjwa huchangamana na wale wazima na hivyo kusababisha maambukizi kusambaa,” Masija anabainisha.
Hali kadhalika, wafanyabishara hao, hutumia fursa hiyo kutorosha wanyama wengine, hali inayoibua mtafaruku kati ya jamii za wafugaji zinazoishi katika mpaka wa Namanga.
Hata hivyo, Masija anaishukuru serikali ya Tanzania kwa maamuzi ya kuvifungia viwanda vya kuchinja punda, vilivyokuwa katika mikoa ya Dodoma na Shinyanga, kwa kukiuka maelekezo ya vibali walivyopewa.
Kulingana na Masija, viwanda hivyo vilipewa ruhusa ya kuchinja punda 30 kwa siku, lakini wao wakaamua kuchinja wanyama 100 kwa siku.