Kuna ulazima wowote kwa bibi harusi kuvaa shela jeupe?
AFRIKA
4 dk kusoma
Kuna ulazima wowote kwa bibi harusi kuvaa shela jeupe?Shela nyeupe ilianza kama ishara ya mtindo wa kifalme na likawa alama ya kitamaduni ya usafi na tabia njema. Hata hivyo, mambo yamebadilika.
magauni ya bi harusi yanakuwa nyeupe mara nyingi / Zenayla Bridal / TRT Afrika Swahili
27 Agosti 2025

Na Dayo Yussuf

Zeynab Deen ni mfanyabiashara anayeuza magauni ya harusi jijini Nairobi. Kwa sasa, ana miliki duka dogo lililonakshiwa na mapambo ya harusini.

‘‘Wanaume mna bahati sana, hamna makubwa katika kuchagua vazi la harusi,’’ anacheka. ‘‘Bora mpate suti au hata mkivaa kingine chochote watu hawajali, bora umependeza.’’

Zeynab amefanya biashara hii kwa takriban miaka minne tangu alipojiuzulu kazi yake ya uandishi.

‘‘Nimejionea mabibi harusi wengi…wakija na wazazi wao na dada zao kuchagua mashela. Wengine wanachagua mashela mitandaoni, hususani kwenye kurasa za Instagram na Tiktok. Gauni jeupe ndio maarufu sana. Ni kama utamaduni unaondelezwa,’’ anaiambia TRT Afrika.

Hadhi yake ya kifalme

Inadaiwa kuwa, utamaduni wa kuvaa shela jeupe, ulianzia kwa Malkia Victoria wa Uingereza. Wakati akifunga ndoa na mwanafalme Albert, mwaka 1840, Victoria alichagua vazi jeupe lenye hariri iliyopambwa na nashki mbalimbali.

Halikuwa jambo la kawaida kwa wakati huo, kwani bibi harusi angevaa vazi lolote alipandalo.

Wakati mabibi harusi wangevaa mavazi yao bila kujali rangi.

Gauni lake jeupe liliashiria usafi na utajiri (kitambaa cheupe kilikuwa kigumu zaidi kudumisha na ghali zaidi), na kutokana na hadhi yake ya kimalkia, iliweka mwelekeo mpya wa mtindo ambao ulienea haraka katika tamaduni za Magharibi.

Na wazo hili lilipokewa na vizazi kwa karne zilizofuata. Baadhi walichukulia kwa hadhi kubwa zaidi hata makanisa yangekataa kuongoza hafla ya kufunga ndoa iwapo bibi harusi hakuwa msichana au mwanamwali.

Mabadiliko yaonekana

Na njia rahisi kuonesha hili ilikuwa ni kuvaa gauni jeupe.

Lakini kadri miaka inavyokwenda, mabadiliko yanaanza kuonekana.

Baadhi ya maharusi wanaonekana kupendelea rangi tofauti zenye kuonesha utu wao, utamaduni, imani au wengine basi tu ukaidi waonekane wamevunja mila ya kigeni.

‘‘Vijana wa leo wanavaa rangi za kila aina, wengine zaidi ya rangi moja, wengine mavazi ya kitamaduni kuonyesha kuwa kusema 'I do,' siku ya ndoa haihusiani na rangi yake ya gauni,’’ anasema Zeynab.

Jukumu la Makanisa

Huku wengine, wakihisi kuonesha iwapo bi harusi ni msichana ni suala la faragha zaidi na halitakiwi kuwekwa wazi.

‘‘Mimi ni muislamu na mara nyingi ma bibi harusi wa kiislamu huvaa nguo ya kijani wakati wa ‘nikaha’, na mimi pia nilivaa vivyo hivyo,’’ anasema Samira Yussuf ambaye aliolewa mwezi Februari mjini Mombasa. ‘‘Lakini baada ya ‘nikaha’ nilivaa shela jeupe kwenda ukumbini.’’

Wakati mwingine vazi leupe harusini lilitiliwa mkazo zaidi kiasi kwamba baadhi ya makanisa yangekataa kuongoza sherehe ya kufunga ndoa iwapo bibi harusi hakuvaa gauni nyeupe.

‘‘Rafiki zangu wakristu wengi wameniambia walivaa gauni nyeupe ili kasisi aruhusu ndoa kufanyika kanisani. Lakini sio wote, mimi nimehudhuria harusi mbili ambazo bi harusi walivaa kitamaduni ya kiafrika, ilipendeza sana,’’ Samira anakumbuka.

Mavazi ya kipekee

Lakini wataalamu wa mitindo wanasema, haijalishi nguo au mshono utakaochagua kuvaa siku ya harusi, muhimu ni kwamba, hiyo ni siku yako, na una uhuru wa kuchagua mtindo unaotaka.

Zeynab anasema kuwa wanawali wanaokuja sasa wengi wanapendelea kuvaa kitu cha aina ya kipekee, na gauni nyeupe ni kitu kimevaliwa tangu mabibi zao kwa hiyo hawazitaki.

‘‘Wanakuambia hawataki harusi ya karne ya kumi na tisa. Mambo ya kisasa ni kutafuta kitu ambacho hakijaonekana bado. Lakini wengine wanasema hawataki kuwekewa masharti kwenye harusi yao, kwa hiyo hawafuati mitindo iliyoambatanishwa na imani za kizamani,’’ anasema Zeynab.

Mfano, imani kuwa anayevaa nyeupe bado ni mwanamwali imezua mjadala mkubwa na pengine hata kuwasukuma baadhi ya maharusi kukataa nyeupe.

Ishara ya mtindo wa kifalme

Vile vile kuna baadhi ya imani ambazo zinawatarajia maharusi kutovaa nyeupe.

Mfano kwa mila za Kihindu, vazi nyeupe huvaliwana mke aliyefiwa na mumewe. Kwa hiyo wanaepuk akuvaa nyeupe siku ya harusi na badala yake wanapendelea nyekundu. Jamii za Kichina pia huvaa nyekundu harusini.

Kimsingi, gauni jeupe la harusi lilianza kama ishara ya mtindo wa kifalme na likakua alama ya kitamaduni ya usafi na tabia njema. Ingawa inaendelea kuwa na maana kwa wengi, pia imetelekezwa na wanaharusi wa kisasa ambao hutanguliza umuhimu wa kibinafsi na utofauti katika mila ya harusi.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us