Hisia tofauti Rais Samia wa Tanzania akitimiza miaka minne madarakani
SIASA
4 dk kusoma
Hisia tofauti Rais Samia wa Tanzania akitimiza miaka minne madarakaniKiongozi huyo, ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, aliapishwa Machi 19, 2021 kuongoza taifa hilo la Afrika Mashariki, kufuatia kifo cha ghafla cha Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais Samia Suluhu Hassan alikula kiapo cha kuiongoza nchi hiyo kufuatia kifo cha ghafla cha Dkt. John Pombe Magufuli./Picha:@ikulumawasliano / Others
24 Machi 2025

“Kwa wale ambao wana mashaka kwamba Mwanamke huyu ataweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka niwaambie aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye maumbile yake ni Mwanamke.”

Ni kauli iliyotolewa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Machi 22, 2021 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma katika hafla ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Rais Samia alitoa kauli hiyo kama ishara ya kuwaondoa hofu wenye mashaka na iwapo angeweza kuimudu nafasi hiyo, hususani ikiwa ni kwa mara ya kwanza, Tanzania kuongozwa na rais mwanamke.

Kiongozi huyo, ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, aliapishwa Machi 19, 2021 kuongoza taifa hilo la Afrika Mashariki, kufuatia kifo cha ghafla cha Dkt. Magufuli, ambaye alikuwa ametumikia mwaka mmoja wa muhula wake wa pili wa uongozi wa awamu ya tano.

Mara tu baada ya kuingia madarakani, kati ya mambo kadhaa yaliyoahidiwa na Rais Samia ni pamoja kuendeleza miradi iliyoachwa na mtangulizi wake, kuruhusu kukosolewa kwa serikali japo kwa staha, na hata kwenda mbali zaidi na kusema yuko tayari kuonana na vyama vya siasa.

Akiwa madarakani, Rais Samia alizindua falsafa yake ya R nne (4R), alizotumia katika utawala wake, akisisitiza maridhiano, mabadiliko ustahimilivu na kujenga upya.

Mawazo mseto

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa mambo ya kisiasa na kijamii nchini Tanzania, wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na miaka minne ya Rais Samia madarakani.

Akiangazia mpango wa Tanzania wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Wanawake (2022-2032) katika mahojiano yake na TRT Afrika, mtafiti na mchambuzi wa masuala ya haki, usawa na jinsia kutoka Tanzania, Deogratius Temba amepongeza mpango huo wenye kulenga kuwapunguzia wanawake wa Tanzania mzigo wa majukumu ya uzalishaji wa chaku la kwa njia zisizo kama kuni na mkaa.

“Mpango huu utaondoa tatizo la ukatili wa kijinsia kwa wanawake ambao ni wapishi kiasili na ndio wanaotakiwa kwenda kutafuta kuni porini, itaondoa tatizo la kiafya kwa wanawake wanaotumia nishati isiyo safi kama kuni na mkaa,”anaeleza.

Ni imani yake kuwa mpango huo utachangia kulinda mazingira kupitia kupunguza ukataji miti na hivyo kujihakikishia upatikanaji wa rasilimali ya maji.

Hata hivyo, Temba ana mapendekezo kadhaa kuhusiana na mkakati huo chini ya uongozi wa Rais Samia.

“Nadhani itakuwa vyema serikali ikatenga fedha za kuruzuku gesi ya kupikia, au kuondoa kodi kwenye gesi ili kuwezesha kupungua kwa bei,” anasema.

Gharama za nishati ya gesi

Kulingana na mchambuzi huyo, gharama za nishati ya gesi bado ziko juu, huku wanawake wa vijijini wakishindwa kumudu kujaza mitungi wanayopewa.

Kwa sasa, gharama za kujaza mtungi wa kilo sita ni Dola 9 za Kimarekani kwa mkoa wa Dar es Salaam, wakati kwa maeneo ya vijijini, wanawake hao watalazimika kulipa hadi Dola 11.

“Katika bajeti ya mwaka 2025/26, Rais Samia angeweka ruzuku kwenye gesi ili kuondoa changamoto hiyo, nina uhakika mkakati huu wa nishati safi utafanikiwa kwa asilimia 100,” anaeleza.

Kuelekea uchaguzi mkuu

Wakati imebaki takribani miezi sita, kabla ya Watanzania hawajafanya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Temba amepongeza Sheria za Uchaguzi (Marekebisho ya 2024) Sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na marekebisho ya Sheria ya mambo ya vyama vya siasa, akisema kuwa mabadiliko hayo yataongeza uwazi, usawa wa kijinsia, na ulinzi wa haki za wanawake na makundi maalum wakati wa uchaguzi.

“Kuna maboresho kwenye taratibu za uteuzi wa wagombea wanawake, usimamizi wa haki zao, na kudhibiti lugha za chuki na ukatili wa kisiasa dhidi ya wanawake,” Temba anaongeza.

Mbali na kupongeza hatua ya Rais Samia kukamilisha miradi ya mtangulizi wake, kama vile mradi wa reli ya kisasa ya SGR, mradi wa kuzalisha umeme katika bwawa la Rufiji, maarufu kama Julius Nyerere Hydropower Plant (JNHPP), Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Msaada wa Kisheria ya CiLAO, Charles Odero anasema bado kuna mambo mengi ambayo kiongozi huyo anapaswa kutupia jicho, wakati akijiandaa kugombea Urais mwezi Oktoba.

“Miaka minne ya Samia kwenye haki za Binadamu ni miaka ya kulia na kusaga meno kwani tumeshuhuhudia utekaji, watu kupotea, kuuwawa,” Odero anaeleza.

Pia anaongeza kuwa kipindi hicho cha miaka minne, pia kimeshuhudia uvurugwaji wa mchakato wa serikali za mitaa.

 Kazi iendelee

Akizungumza Machi 17, 2025 jijini Mbeya, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Steven Wasira alisema kuwa kupitia kauli yake ya ‘kazi iendelee’, Rais Samia ametekeleza miradi mikubwa ya kimkakati nchini humo.

“Kazi imendelea tena kuliko wengine tulivyodhani , nitawapa mifano michache, moja wakati Dkt. Magufuli anaondoka duniani alianzisha ujenzi wa reli ilikuwa imefika Morogoro lakini ilikuwa haijakamilika ,Rais Samia ameendeleza reli ya SGR sasa imefika Makutupola mkoani Singida,leo Dar es Salaam na Morogoro mpaka Dodoma imekuwa karibu kwasababu ya reli hii,”alisema Wasira.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us