Uchambuzi: Kwa nini Bahari ya Kaspi inasababisha mtafaruku
SIASA
10 dk kusoma
Uchambuzi: Kwa nini Bahari ya Kaspi inasababisha mtafarukuSehemu ya Kaspi inatambulika kama bahari. Hata hivyo, rasilimali zake za madini hazijagawanywa kikamilifu - suala hili liliachwa kwa makubaliano ya pande mbili zinazopakana na bahari hiyo.
Meli za jeshi la wanamaji wa Azerbaijan na Iran wakifanya mazoezi ya pamoja kwenye Bahari ya Kaspi, nchini Iran, picha iliyopatikana 4 Novemba, 2024. Picha: Reuters / Reuters
9 Machi 2025

Maji tulivu ya Bahari ya Kaspi yanatoa ishara siyo tu ya ufukwe wa mataifa matano, bali pia matarajio, matumaini, na mikakati yao.

Eneo hili la kale, ambalo ni ziwa kubwa zaidi duniani, limekuwa sehemu ya siasa za dunia, ambapo kuna maslahi ya nchi zenye uwezo, njia za nishati, na changamoto za kisheria zinakuwepo pamoja.

Zaidi ya semantiki: Bahari au ziwa?

Tangu kusambaratika muungano wa Sovyeti mwaka 1991, mataifa matano ya Kaspi—Azerbaijan, Iran, Kazakhstan, Urusi, na Turkmenistan—yameshindwa kufikia makubaliano ya kisheria kuhusu Kaspi. Swali linaloonekana rahisi: Je, ni bahari au ziwa? Hata hivyo, swali hili linaamua hatima ya matrilioni ya kiwango cha gesi. mabilioni ya mapipa ya mafuta, ushoroba muhimu wa usafirishaji.

Ikiwa Kaspi ni ziwa, basi sehemu lazima igawanywe sawa miongoni mwa mataifa yote matano. Kama ni bahari, basi Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sheria ya Bahari unatumika, ambapo mgawanyo unafuata kanuni ya urefu wa ukanda wa pwani.

Katika hali hii, Kazakhstan, yenye ukanda mrefu zaidi wa pwani, inapata sehemu kubwa zaidi, huku Iran, yenye ukanda mdogo wa pwani, ikipata sehemu ndogo.

Katika sintofahamu hii ya kisheria, kila nchi ilitetea msimamo unaolinda zaidi maslahi yake. Iran ilisisitiza kwamba Kaspi ifahamike kama ziwa, jambo ambalo lingewapa asilimia 20 sawa ya rasilimali na mataifa mengine.

Azerbaijan, Kazakhstan, na Turkmenistan zilipendelea iwe ni bahari, ambapo ingeongeza sehemu zao kulingana na urefu wa ukanda wao wa pwani.

Urusi imekuwa na msimamo tofauti, ikikataa tafsiri zote mbili, kwani kutambua Kaspi kama bahari kungeilazimisha kuruhusu meli za kigeni kupitia Mto Volga, kinyume na maslahi yake ya kimkakati.

Kabla ya kusambaratika kwa muungano wa Sovyeti, makubaliano ya pande mbili kati ya Sovyeti na Iran yalifafanua sheria za kufanya shughuli pamoja na biashara katika Kaspi, ambayo kimsingi ilikuwa imefungwa kwa mataifa ya tatu.

Kuibuka kwa mataifa mapya huru kulibadilisha kabisa ramani ya kisiasa ya eneo hilo, na kufanya suala la kuhusu Kaspi kuwa la mgogoro wa pande nyingi wenye maslahi makubwa.

Hazina ya nishati

Maslahi ni mapana kwa kweli. Makadirio yanaonesha kuwa bahari ya Kaspi ina mapipa bilioni 48 ya mafuta na kiwango kikubwa zaidi cha gesi asilia. Eneo hilo pia lina samaki wenye thamani wa sturgeon, ambao huzalisha baadhi ya mayai ghali ya samaki duniani.

Kutokuwa na utambuzi maalum wa Kaspi kunasababisha changamoto katika kuimarisha utajiri huu kwa miongo kadhaa. Hasa kuhusu raslimali zinazopatikana Kusini mwa Kaspi, ambapo Azerbaijan, Iran, na Turkmenistan wanadai kuwa ni zao. Migogoro miwili mikubwa kuhusu mipaka iliibuka: Mgogoro kati ya Turkmenistan na Azerbaijan kuhusu sehemu ya "Serdar-Kapaz", kati ya Azerbaijan na Iran ambapo wao wanatambuwa kama "Araz-Alov-Sharg" .

Wakati mwingine migogoro hii inaibua hali ya hatari. Mapema katika miaka ya 2000, uhasama kati ya Iran na Azerbaijan kuhusu maeneo yenye migogoro ya Kaspi ulirindima:

Iran ilitishia kuzishambulia meli mbili za Azerbaijan ambazo zilikuwa zinafanya utafiti kwa niaba ya shirika la mafuta la British Petroleum, kulazimisha zirejee kwao, na kuondoa mipaka ya baharini iliyowekwa na Azerbaijan.

Waziri Mkuu wa Azerbaijan Artur Rasizade alieleza kutoridhishwa na hatua hiyo kwa balozi wa Iran Ahad Ghazai na kutaka maelezo kuhusu jambo hilo.

Hali ikawa mbaya zaidi mwaka 2001 wakati wapiganaji wa Iran walipokiuka sheria za anga ya Azerbaijani mara zisizopungua nane, kuingia ndani zaidi (hadi kilomita 100-180 kutoka Baku) na kupaisha ndege sehemu ya karibu na makazi ya watu nchini Azerbaijani.

Katika wakati huu muhimu, Uturuki iliingilia mzozo huu, kwa kuwasaidia Azerbaijan kwa njia ya kijeshi na kisiasa. Baada ya Uturuki kuonesha uwezo wao, ikiwemo kupeleka ndege za kivita za "Uturuki za Falcon" hadi Azerbaijan 24 Agosti 2001, ukiukwaji wa Iran kwa mipaka ya Azerbaijan ukasitishwa. 

Iran ilijitetea kuwa walifanya hivyo kutokana na kutokukubaliana na kugawanywa kwa sehemu Sovieti ya Kaspi miongoni mwa mataifa manne.Iran ilitaka asilimia 20 ya bahari kwa ajili yao, bila kuzingatia urefu wa bahari au haki za kihistoria.

Safari ndefu ya kufikia makubaliano

Mataifa ya Kaspi yalianza kujadili mfumo wa kisheria wa Kaspi 2002 katika mkutano wa kwanza katika mji mkuuwa Turkmenistan, Ashgabat. Alafu kukawa na mikutano mingine mjini Tehran 2007, Baku 2010, na Astrakhan 2014. Kila mkutano ulileta mataifa haya karibu kufikia makubaliano, lakini makubaliano hasa yalifikiwa 12 Agosti, 2018.

Katika mji wa Kazakhstan wa Aktau, viongozi wa mataifa ya Kaspi walitia saini makubaliano kuhusu hadhi ya kisheria ya Bahari ya Kaspi. Vladimir Putin aliyataja makubaliano hayo kama "mabadiliko makubwa," ilhali Rais wa Kazakhstan Nursultan Nazarbayev akisema kuwa ni "Katiba ya Kaspi”

Makubaliano hayo yaliashiria kuafikiana kwa aina fulani, huku kila mmoja akiachana na msimamo mkali, jambo la kawaida katika masuala ya kimataifa. Kaspi haikutajwa kama ni bahari au ziwa, lakini kama "sehemu ya maji yenye hadhi maalum kisheria" (hati hiyo ilitumia neno "Bahari ya Kaspi," lakini kifungu cha 1 kimeeleza tu kama "sehemu ya maji"). Uamuzi huu umefanya kusiwepo na sheria ya kimataifa ambayo inahusisha bahari au maziwa, kufanya kuwepo kwa utata wa kisheria na kusababisha hali kuwa kama ilivyo.

Kulingana na hati hiyo, sehemu ya Kaslpi inatambulika kama bahari: Mataifa yana uhuru wa eneo hadi maili kumi na tano nm kutoka kwenye fukwe zao na nm 10 zaidi kwa ajili ya haki za uvuvi. Hata hivyo, raslimali ya madini haikugawanya - hili liliwachwa kwa ajili ya makubaliano ya pande mbili. Kwa ufupi, mkutano huo haukutowa suluhu yoyote kuhusu tatizo hilo, ikawa ni kama kuthibitisha hali ilivyo kwa sasa.

Makubaliano hayo yaliweka sheria muhimu: meli za kijeshi ambazo hazitoki katika mataifa ya Kaspi haziruhusiwi kuwa katika maeneo ya maji ya Kaspi. Zaidi, mataifa yaliyokubaliana hayawezi kutoa ruhusu kwa nchi zingine kutumia eneo lake katika mashambulizi dhidi ya mataifa yaliyoorodheshwa kwenye makubaliano hayo. Kanuni hizi za makubaliano za kijeshi zinaendana na maslahi ya Urusi na Iran, wakihofia kuwepo kwa vikosi vya NATO katika eneo hilo.

Kutoka kwa mtazamo wa Azerbaijan, Kazakhstan, na Turkmenistan, kuwepo kwa eneo lisilo na wanajeshi itakuwa muhimu, lakini Urusi imekuwa ikikataa hilo. Hasa kutokana na kuwa manowari za kijeshi za Urusi zimefanya mashambulizi nchini Syria na Ukraine kutoka Bahari ya Kaspi inaonesha umuhimu wa kijeshi wa bahari hiyo kwa Urusi.

Mkataba wa kijeshi una athari kubwa zaidi kwa kudhihirisha uwezo katika kanda hiyo. Marufuku ya kutokuwepo kwa wanajeshi hapo na kutumia sehemu hiyo kwa ajili ya mashambuli dhidi ya mataifa ya Kaspi, kunawapa Urusi faida, kwa kuwa wana meli nyingi zaidi katika eneo la Kaspi. Matokeo yake, Azerbaijan, Kazakhstan, na Turkmenistan hawana uwezo wa kuvutia washirika kwa ajili ya ushirikiano wa kijeshi kwenye eneo hilo.

Hili linadhoofisha uwezo wao wa kujadiliana kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta, kwa kuwa wanakabiliwa na majirani wenye uwezo mkubwa wa kijeshi bila ya usaidizi kutoka nje wakati panapokuwa na mzozo. Kwa hiyo, kupatikana kwa usaidizi wa kijeshi kama sehemu ya mkataba huo inakuwa njia muhimu ya kutatua masuala ya kiuchumi na mipaka katika eneo hilo.

Bomba la mafuta la Kaspi: linawezekana au ni ndoto tu?

Moja ya masuala tata kuhusu Kaspi inahusiana na ujenzi wa bomba la mafuta linalounganisha Turkmenistan na Azerbaijan. TMradi huu, kwanza ulipendekezwa miaka ya 90, na utaruhusu Turkmenistan,taifa la nne kwa ukubwa wa hifadhi ya mafuta duniani, kusambaza raslimali za nishati barani Ulaya bila kutegemea Urusi — mpango uliotiliwa nguvu na nchi za Ulaya ambazo zilitaka kuondokana na utegemezi wa gesi kutoka Urusi.

Mkataba wa 2018 uliruhusu ujenzi wa bomba la mafuta chini ya bahari,ikihitaji ruhusa kutoka kwa mataifa ambayo bomba hili linapita tu. Waraka huo pia una vipengele vya uhifadhi wa mazingira ambavyo vinaweza kutumiwa kuzuia mradi kama huo.

Urusi, yenye lengo ya kubaki kuwa muuza gesi mkubwa barani Ulaya,imekuwa ikipinga bomba hilo la Kaspi, kwa kutaja sababu za hatari kwa mazingira.

Njia mpya na uhalisia wa mambo

Tarehe 1 Machi, 2025, jambo kubwa lilifanyika: Gesi ya Turkmenistan ilianza kuingia Uturuki kupitia Iran kufwatia mpango wa kubadilishana miradi. Makubaliano ni kufikisha hadi ujazo wa ‘cubic meters’ bilioni mbili kwa mwaka, kukiwa na matarajio ya kuongeza hadi bilioni 15. Hii ilitokana na majadiliano ya muda mrefu kati ya Turkmenistan, Iran, na Uturuki.

Mpango huu wa kubadilishana miradi unafanya kazi hivi: Gesi ya Turkmenistan inaingia Iran, na Iran inatua kiwango sawa na hichi kwa Uturuki. Kisheria, hii inakuwa gesi ya Turkmenistan, kuepukana na vikwazo vya kimataifa vilivyowekwa dhidi ya.

Hata hivyo, Uturuki pia ina mpango wa kupata gesi ya Turkmenistan kupitia Azerbaijan na Georgia. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kufikishwa kwa gesi kutoka Turkmenistan hadi Uturuki na Ulaya,pamoja na kuongeza uwezo wa bomba la mafuta la TANAP ni jambo litakalofanyika "hivi karibuni”

Kutumia njia hii kunahitaji ujenzi wa bomba chini ya bahari ya Kaspi. Na ndiyo hapa tunarudi kwenye tatizo la hadhi ya Kaspi.

Hali ya mzozo kwa sasa

Licha ya kutia saini mkataba wa 2018, baadhi ya masuala bado hayajatatuliwa. Mkataba huo uliweka kanuni za kwa ujumla,lakini kugawanywa kwa maeneo ya bahari bado inahitaji makubaliano ya mataifa mawili.

Upande wa kaskazini wa bahari ya Kaspi kulikuwa kumegawanywa kati ya Urusi, Kazakhstan na Azerbaijan kulingana na makubaliano ya 2001 na 2003. Lakini mizozo ya kimipaka kati ya Azerbaijan, Iran, na Turkmenistan bado inaendelea Kusini mwa Kaspi.

Baada ya kutiwa saini kwa makubaliano, raia wengi wa Iran waliishtumu serikali yao kwa "kuuza" Kaspi, huku sehemu ya Iran ikiwa ni ndogo kuliko kama kungekuwa na mgao wa sawa sawa. Rais wa Iran Hassan Rouhani alisisitiza kuwa makubaliano zaidi yatahitajika katika kugawanya sehemu ya bahari.

Sehemu ya Kaspi na siasa za dunia

Tofauti kuhusu hadhi ya Kaspi zinaendelea hata nje ya maslahi ya kanda hii. Inaathiri upatikanaji wa nishati duniani, ushindani kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi, na kuongezeka kwa ushawishi wa China Katikati mwa Asia.

Marekani na Umoja wa Ulaya wanaunga mkono kuwepo kwa njia nyingi za kupitisha nishati na kuacha kutegemea gesi ya Urusi. Kwa hiyo, wana nia ya kutekeleza utumiaji wa bomba la Kaspi na miradi mingine ambayo ingesafirisha raslimali za nishati za Katikati mwa Asia hadi katika soko la Magharibi bila kutegemea Urusi.

Wakati huohuo China, imekuwa muagizaji mkubwa wa gesi ya Turkmenistan kupitia mabomba ya Katika mwa Asia na China. China ina mpango ya kuimarisha nafasi yake katika kanda hiyo kupitia mradi wa ‘‘Belt and Road Initiative."

Urusi na Iran, ambao wanakabiliana na vikwazo kutoka kwa mataifa ya Magharibi, wanaimarisha ushirikiano wao wa kimkakati huku wakijaribu kuhakikisha ushawishi wao kenye Kaspi. Mkataba wa 2018, kuzuia kuwepo kwa wanajeshi wasio wa kanda hiyo, unaendana na maslahi yao.

Mustakabali wa Kaspi

Kuimarisha mataifa ya Kaspi na kubadilisha kwa siasa za dunia kunaweza kufanya kuwepo kwa makubaliano mapya kuhusu masuala tata ya Kaspi. Inawezekana kuwa mkataba wa 2018, pamoja na kuwa haikuangalia masuala yote kwa kina, ulikuwa msingi muhimu kwa majadliano katika siku za baadaye.

Mradi wa bomba la mafuta la Kaspi bado unawezekana, hasa kutokana na azma ya Ulaya ya kuwa na njia mbadala ya kusambaza nishati na nia ya Turkmenistan kuongeza njia za kusafirisha nishati yao nje ya nchi. Hata hivyo, utekelezaji wake unategemea namna ya kuoanisha maslahi ya kiuchumi, kuzingatia mazingira, na siasa za dunia.

Usambazaji wa gesi ya Turkmenistan hadi Uturuki kupitia Iran inaonesha suluhu la uhakika hata wakati kukiwa na vikwazo na wasiwasi katika kanda. Mpango huu unaweza kutumika kama mfano wa miradi mingine katika kanda hiyo.

Kwa vyovyote vile, hatima ya Kaspi na utajiri wake itatatuliwa siyo na mifumo ya kisheria lakini na uwezo wa mataifa husika yatakayofikia makubaliano katika karne hii ya 21 yenye misukosuko.

Kama alivyosema rais wa Kazakhstan, mkataba kuhusu hadhi ya kisheria ya Kaspi imekuwa kama "Katiba ya Kaspi." Na sawa na katiba nyingine yoyote, inaweza kuwa msingi wa kuimarisha uhusiano zaidi. Pengine siyo wote ambao' malengo yao yatatoshelezwa, lakini msingi umewekwa kwa ajili ya kushirikiana kwa amani na utumiaji wa pamoja wa utajiri ulioko kwenye sehemu hii ya maji.

Wakati huohuo, huku mataifa makubwa yakiendelea na mambo yao, Kaspi, ambayo imekuwepo kwa maelfu ya miaka, maji yake ni kati ya bara Asia na Ulaya, siyo tu ina hazina kubwa ya nishati, lakini pia ustaarabu wa kale tangu enzi ambao ulikuwepo kwenye fukwe zake miaka mingi kabla mafuta na gesi kuanza kuwa sehemu ya hatima ya mataifa yao.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us