Bajuni: Jamii inayopambana kuhifadhi urithi wake wa lugha na utamaduni
MAISHA
3 dk kusoma
Bajuni: Jamii inayopambana kuhifadhi urithi wake wa lugha na utamaduniKutokana na asili yake ya Kibantu, lahaja ya Kibajuni imeazima maneno mengi kutoka lugha za Kiarabu na Kiafrika, ikionyesha muingiliano wa kitamaduni na biashara kati ya Wabajuni na jamii za pwani.
"Wabajuni kama wanavyofahamika ni jamii iliyo na asili yake katika visiwa vya Bajuni, pwani ya Somalia/ Picha : TRT Afrika" / TRT Afrika Swahili
28 Novemba 2024

Na Mustafa Abdulkadir

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

‘’Ambacha ukucha punda uyao!’’

Kama umewahi kubahatika kutembelea visiwa vya Lamu, Pwani ya Kenya, utajua maana ya maneno hayo. Ni onyo kuwa upo katika hatari ya kugongwa na punda anayepita kwa kasi katika vichochoro vya mji wa Lamu.

Lakini hicho ni Kiswahili? Naam. Kibajuni haswa. Wana namna yao ya kutamka maneno ya Kiswahili kwa lahaja ya kipekee. Hata ukiwa mjuzi wa Kiswahili kiasi gani, ukimsikia Mbajuni akizungumza, utaachwa mdomo wazi kwa utamu wake.

Wabajuni kama wanavyofahamika ni jamii iliyo na asili yake katika visiwa vya Bajuni, pwani ya Somalia, japo kutokana na uhamiaji wa miaka mingi wanapatikana katika pwani ya Kenya na baadhi nchini Tanzania.

Kutokana na asili yake ya Kibantu, lahaja ya Kibajuni imechukua maneno mengi kutoka lugha za Kiarabu na Kiafrika, ikionyesha mwingiliano wa kitamaduni na biashara kati ya Wabajuni na jamii za pwani.

Changamoto si haba

Hata hivyo, utamaduni na lugha ya Wabajuni unakabiliwa na changamoto za kisasa na mabadiliko ya mazingira. Kwa kujibu changamoto hizo, vitabu vya lahaja ya Kibajuni vimezinduliwa kwa mara ya kwanza mwezi Machi kisiwani Lamu, Pwani ya Kenya.

“Pamoja na kitabu kilichozinduliwa ni kitabu kinachoitwa ‘Bajuni, Land, Language and Orature’, kina insha sita na kinazungumzia turathi za kibajuni,’’ anasema Profesa Kimani Njogu, Mkurugenzi wa Shirika la Twaweza Communications lililohusika katika uchapishaji wa vitabu hivyo.

‘’Kimetafsiriwa kwa Kiingereza na lengo la kitabu hicho ni kuingiza taaluma katika masuala ya kibajuni, katika akademiya kimataifa,” anaiambia TRT Afrika.

Vitabu hivyo ni pamoja na kitabu cha “Mashairi ya Kibajuni” kilichohaririwa na Omar Lali na Omar Maulana, kitabu cha ‘Shivulani ni Shaulani’ kilichoandikwa na Mohamed M. Kombo, na kitabu cha ‘Chusomeni Kibajuni’ cha gredi ya 1, 2 na 3, kilichoandikwa na Yumna Hadid Titi akishirikiana na Fuad Aroi na Yumbe Athman.

Wahusika wa machapisho haya wanapendekeza vitabu hivi vijumuishwe katika mtaala wa elimu ya msingi nchini Kenya kama njia ya kupitisha kwa vizazi vichanga.

‘’Tumeomba idhini kutoka Wizara ya Elimu vitabu hivi viongezwe katika mfumo wa elimu katika kitengo cha lugha ya kiasili katika madarasa ya gredi 1,2, 3. Tunasubiri mwongozo wa Wizara ya Elimu,’’ anaongeza Profesa Njogu.

‘’Ulilikacha Shauri, Ikakudhidi kiburi, Ukiambiwa subiri, Hukuivona hatari, Na kwa sasa ndahiyari, Uliiata bandari…….’’

Dondoo kutoka shairi ‘Nvuli na Nkewe, lililoandikwa na Abdallah Ali.

Utajiri wa Kitamaduni

Mbali na lugha, Wabajuni pia wanajisifia utamaduni ulio mpana.

Ustadi wa Wabajuni katika ufundi wa majahazi na usindikaji wa samaki umewaletea umaarufu, huku ngoma na nyimbo zao zikionyesha utajiri wa utamaduni wao katika sherehe za kitamaduni na matukio muhimu.

“Uzinduzi wa vitabu hivyo ni hatua muhimu katika kuhifadhi utamaduni wa Kibajuni na kuwapa fursa watoto kujifunza na kuendeleza lahaja yao,’’ Profesa Njogu anaiambia TRT Afrika.

Idadi kamili ya Wabajuni haijulikani kutokana na uhamiaji mkubwa, lakini inaaminiwa kuwa takriban watu 300,000 bado wapo katika visiwa vya pwani ya Somalia, Kenya na Tanzania.

Na uchapishaji wa vitabu hivi unatazamiwa kuwaweka Wabajuni katika ramani ya Kimataifa.

“Lengo la uzinduzi wa vitabu hivyo ni kutoa fursa kwa washairi wa Kibajuni kupata sifa kimataifa na kuwaonyesha kuwa wapo na wanachangia katika uundaji wa kazi za fasihi. Vitabu hivyo pia vinalenga kuingiza taaluma ya Kibajuni katika akademiya kimataifa," anasema Profesa Njogu.


CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us