Eneo la Nyala la Sudan ndiko kulikofanyika sherehe Agosti 31 ambayo itabadilisha muelekeo wa taifa lililokumbwa na mapigano, yaliyochochewa na mfarakano wa kisiasa kuwahi kutokeo tangu kujiondoa kwa Sudan Kusini.
Mohamed Hamdan Dagalo, kiongozi wa wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) ambao wamekuwa wakipigana na jeshi la Sudan (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan tangu Aprili 2023, alikula kiapo siku hiyo kama mkuu wa serikali pinzani.
Kiongozi wa wapiganaji Abdelaziz Adam al-Hilu, aliapishwa kama naibu wa Dagalo, na baraza la watu 13 linakamilisha utawala huo, kulingana na taarifa kutoka kwa muungano huo mpya wa Sudan.
Wakati wa kuundwa kwa serikali hiyo unaonekana kupangwa mahsusi kwenda sanjari na hafla iliyokuwa inaendelea kwa upande wa wapinzani wao. Siku chahe kabla, serikali inayoongozwa na al-Burhan, ilifanya mkutano wake wa kwanza wa baraza la mawaziri mjini Khartoum tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Sasa, kukiwa na serikali mbili pinzani, wataalamu wanaona mgawanyiko wa taifa la tatu lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika kusambaratika. Kuundwa kwa serikali pinzani, ambayo baraza la kijeshi limeitaja kuwa "serikali bandia", pia inaonesha kuwa hakuna upande ambao unakaribia kupata ushindi.
Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wote wamekataa mamlaka ya serikali pinzani nchini Sudan, wakiitaja kama hatari kwa umoja wa nchi na uhuru wake.
Kupigania utawala
Mapigano ya kijeshi yako dhahiri katika eneo la El-Fasher, ambalo limekabiliwa na vita vya kijeshi kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Picha za satelaiti kutoka Maabara ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Yale zinaonesha namna RSF ilivyoweka vizuizi kwa zaidi ya kilomita 31, vilivyozunguka mji na kufungia watu katika sehemu hiyo.
RSF inaweza kutumia serikali pinzani kama jukwaa la ''kuhalalisha'' kuwepo kwake na kutaka kutambulika kimataifa, mwanazuoni wa Sudan Dkt Mayada Kamal Eldeen ameiambia TRT Afrika.
''Hili linaweza kutatiza mapigano na kuanzishwa kwa vita vingine," Dkt Eldeen anasema.
Baadhi ya wachambuzi wanasema hali hii inaweza kusababisha kuwepo kwa makundi ya wapinzani zaidi na kufanya hali kwa watu kuwa mbaya zaidi."
Janga limeongezeka
Huku migogoro ikiendelea, idadi ya watu wanaouawa inaongezeka.
Maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni 14 kuondolewa katika makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa. Mahakama ya Kimataifa imeanzisha uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita na vita dhidi ya ubinadamu.
Katika eneo la El-Fasher pekee, baadhi ya raia 300,000 wamekwama huko, hawana chakula, maji, dawa na misaada.
Wito wa Muungano wa Afrika kwa wadauu "kuacha vita na kuungana katika kutoa misaada ya dharura" unaonekana kutosikika huku vita vikirindima.
Mashirika ya misaada yanajikuta katika njiapanda. Baadhi ya maeneo Sudan hayafikiwi kabisa kutokana na mapigano. Katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi, mashirika ya misaada yanalazimika kukabiliana na hali ngumu ya kufanya kazi na utawala ambao Umoja wa Mataifa hauutambui.